Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WIZARA MPYA TUCHAPE KAZI KWA KASI YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amewataka watumishi wa Wizara yake pamoja na taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kufanya kazi kwa kasi ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan

 

Dkt. Ndugulile ameyasema hayo wakati akifungua mkutano namba 2/2020/2021 wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, Dodoma

 

Amewaeleza wafanyakazi wa Wizara hiyo kuwa wameyasikia maelekezo ya Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa Wizara yetu ikiwemo usimamizi na uendeshaji wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), mikakati ya kufikisha mawasiliano kwenye maeneo ya pembezoni mwa nchi yetu na kuangalia upya suala la mabando na kuweka uratibu mzuri wa utekelezaji wake pamoja na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere ambapo tayari Wizara ilianza kuyatekeleza na kufanyia kazi hivyo ana imani kuwa wataalamu wa Wizara wana majibu yote na ndio umuhimu wa kufanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano

 

Vile vile, amesisitiza kwa wafanyakazi hao kuwa Wizara hii sio ya kwake wala ya menejimenti ya Wizara hiyo bali ni Wizara ya wafanyakazi wote, hivyo wafanyakazi wote wana wajibu wa kutumikia watanzania kuendana na majukumu ya kila mfanyakazi kwa kuongeza kasi zaidi ya kutekeleza majukumu ya Wizara ikizingatiwa kuwa Wizara imeongezewa bajeti kutoka shilingi bilioni kumi na sita kwa mwaka wa fedha wa 2020/21 na kufikia shilingi bilioni 216 kwa mwaka wa fedha wa 2021/22.

 

Pia, amewataka wafanyakazi kuhakikishia wanaongeza kasi ya kuitambulisha Wizara mpya kwa wananchi ili waelewe majukumu ya Wizara kwa kuzingatia kuwa Wizara hii ndiyo yenye dhamana ya masuala ya TEHAMA nchi nzima na inasimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA na Wizara hii ni mtambuka, ni kiungo mchezeshaji kwa kuwa inagusa nyanja ya kijamii, kiuchumi, ulinzi na usalama

 

Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo Andrea Mathew amewaeleza wafanyakazi hao kuwa Serikali ya Awamu ya Tano na ya Sita ni sawa na makocha wa mpira, hivyo kila mmoja awajibike kutekeleza majukumu yake na kuonesha anatosha katika nafasi yake na kuendeleza ushirikiano baina ya wafanyakazi na viongozi ili Wizara iweze kutekeleza majukumu yake kuendana na matakwa ya Serikali ya sasa

 

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa lengo la Mkutano huo ni kutoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa mwaka wa fedha wa 2020/21 na kuwasilisha mpango wa bajeti kwa mwaka 2021/22; mada mbali mbali zinazohusu afya na ustawi wa wafanyakazi mahali pa kazi na kuhimiza viongozi kuzingatia maslahi ya wafanyakazi na kuleta umoja, mshikamano na upendo kazini.

 

Mwenyekiti wa TUGHE wa tawi la Mawasiliano, Laurencia Masigo, akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa Wizara hiyo, amewashukuru viongozi wa Wizara kwa kuchochea amani mahali pa kazi na kuwaomba viongozi kufuatilia mwongozo wa gharama za usafiri wa mabasi kutoka kwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Usafiri Nchi Kavu (LATRA) ili watumishi waweze kulipwa nauli stahiki wakati wa likizo zao na kufuatilia malipo ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi kwa mamlaka husika ili watumishi 19 waliobaki kati ya watumishi 30 waweze kulipwa.