Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WIZARA IKAWE MFANO FURSA ZA KIUCHUMI ZA SEKTA YA MAWASILIANO KITAIFA NA KIMATAIFA- DKT. YONAZI


Na Chedaiwe Msuya, WHMTH, DODOMA

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inakusudia kuwa kitovu cha fursa katika Sekta ya TEHAMA Kitaifa na Kimataifa.

Hayo yamesemwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Jim Yonazi wakati akifungua kikao Kazi cha uchambuzi wa fursa za kiuchumi za Sekta ya Mawasiliano kitaifa na kimataifa jijini Dodoma leo. 

Dkt. Yonazi amesema kuwa  kusudi la kikao kazi hicho ni kuangazia fursa za kisekta zilizopo nchini na mchango wake katika kukuza uchumi wa nchi.
 
Pia, ameongeza kuwa Serikali imelenga kujenga uelewa kwa wananchi kuhusu  fursa zilizopo katika sekta ya Habari, Mawasiliano na TEHAMA ili waweze kutumia vyema fursa zinazokuwa zinajitokeza ndani na nje ya Tanzania.
 
“Serikali imeweza kuweka mikakati ya kuwajengea uwezo watu pamoja na wadau ili kuhakikisha tunakuza sekta hii ya mawasiliano, kama mnavyo fahamu lazima tutekeleze mpango wa maendeleo kwa kuangalia yaliyomo ndani ya nchi yetu pamoja na mambo yanayoweza kuhamasisha,”alisema.
 
Dkt. Yonazi amesema Wizara hiyo ina jukumu la kuchambua na kuangalia ni nchi zipi Tanzania inaweza kushirikiana nazo, lakini pia kuangazia suala la ujenzi wa minara na kuongeza uwezo wa kutumia simu janja pamoja na usalama wa mtandao.

“Tunatakiwa kuwa Wizara ya mfano kwa kupanua wigo wa fursa za kiuchumi na  kuandika historia kwa kuifanya Sekta ya Mawasiliano kuchangia kwa kiwango kikubwa  mabadiliko na mageuzi katika uchumi wa nchi yetu", amesema Dkt. Yonazi

Ameongeza kuwa lengo kubwa la kikao hiki ni kuiwezesha Tanzania kufikia malengo ya kukuza uchumi kupitia TEHAMA sambamba na fursa zingine zilizo kitaifa na kimataifa.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Wizara hiyo, Bwn. Mulembwa Munaku amesema kuwa amepokea maagizo aliyoyatoa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, wataenda kujadili kwa kina na kuona mkakati watakao kuja nao ambao utasaidia TEHAMA kuchangia pato la taifa kwa asilimia 3% ifikapo 2025.