Habari
WIKI YA UTUMISHI WA UMMA 2026 YAFUNGULIWA RASMI, SERIKALI YASISITIZA UWAJIBIKAJI JUMUISHI KWA HUDUMA ENDELEVU
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb) Juni 17, 2026 amefungua rasmi Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, huku Serikali ikisisitiza umuhimu wa uwajibikaji, uwazi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mhe. Kikwete amesema kuwa Watumishi wa Umma wana wajibu wa kuendelea kuimarisha utendaji kazi wenye tija, kuzingatia maadili ya utumishi na kutumia ubunifu katika kuwahudumia wananchi ili kuchochea maendeleo endelevu ya Taifa.
Ameeleza kuwa maadhimisho hayo ni fursa muhimu ya kuonesha mafanikio yaliyopatikana katika utoaji wa huduma za umma, kuimarisha mahusiano kati ya Serikali na wananchi pamoja na kupokea maoni yatakayosaidia kuboresha zaidi huduma zinazotolewa.
Katika maadhimisho hayo, taasisi mbalimbali za umma zikiwemo wizara, wakala na mashirika ya Serikali zinatoa elimu na huduma kwa wananchi kupitia mabanda ya maonesho yaliyopo katika Viwanja vya Chinangali Park.
Mhe. Kikwete pia ametembelea mabanda mbalimbali ya maonesho na kujionea huduma zinazotolewa, huku akiwapongeza watumishi wa umma kwa juhudi zao za kuendelea kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo "Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu," inayolenga kuimarisha ushiriki wa wadau wote katika kuboresha utoaji wa huduma za umma nchini.
