Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAZIRI SILAA AZINDUA MAABARA TANO ZA TEHAMA KATIKA SHULE ZA SEKONDARI IRINGA


Na Mwandishi Wetu, WMTH, Iringa.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe.  Jerry William Silaa (Mb.), amezindua rasmi maabara tano za TEHAMA katika shule tano za sekondari mkoani Iringa, katika hafla iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Nyalumbu, wilayani Kilolo tarehe 10 Juni, 2025.

Maabara zilizozinduliwa ni za Shule za Sekondari Kilolo, Udzungwa, Selebu, Uhambingeto na Nyalumbu.

Waziri Silaa ameeleza kuwa vifaa vya TEHAMA vilivyowezesha kuanzishwa kwa maabara hizo vimetolewa kupitia ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la Reneal International Education Outreach, kwa usaidizi wa Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mhe. Ritta Kabati.

“Ushirikiano huu unaonesha namna sekta binafsi inavyoweza kushirikiana na Serikali katika kuleta mageuzi ya kidijitali, hususan kwa vijana wetu walioko mashuleni,” amesema Waziri Silaa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri Silaa amesema kuwa Wizara anayoiongoza ndiyo yenye dhamana ya kusimamia masuala ya TEHAMA nchini, na kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), inatekeleza miradi mbalimbali inayochagiza ukuaji wa TEHAMA, hususan katika sekta ya elimu.

Aidha, Waziri ameuagiza Mfuko wa UCSAF kuhakikisha walimu wa TEHAMA katika shule hizo wanapatiwa mafunzo maalum ya TEHAMA, ili kuwawezesha kutumia vizuri vifaa vilivyopo kwenye maabara hizo.

Vilevile, ameitaka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kutembelea shule hizo tano na kusaidia kuanzisha klabu za TEHAMA kwa ajili ya wanafunzi, ili kukuza uelewa wao na kuwahamasisha kutumia teknolojia kwa manufaa ya kitaaluma na ubunifu.

Katika hatua nyingine, Waziri Silaa amewaelekeza watendaji wa Wizara kushirikiana na wadau kuhakikisha Shule ya Sekondari Nyalumbu inapatiwa vifaa vya nyongeza ikiwa ni pamoja na printa, mashine ya fotokopi na smart blackboard (ubao wa kisasa wa kidijitali).

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Mhe. Rebecca Sanga Nsemwa, amesema kuwa vijana wa sasa ni watumiaji wakubwa wa teknolojia, na hivyo uwepo wa maabara hizo utaongeza ufanisi wa kujifunza na kuinua kiwango cha ufaulu mashuleni.

Naye Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Iringa (CCM), Mhe. Ritta Kabati, amesema shirika la Reneal limetoa kompyuta mpakato 20 kwa kila maabara, pamoja na seva moja na router moja. 

Amesisitiza kuwa kuna fursa nyingi katika TEHAMA, na kwamba Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuwekeza kikamilifu katika teknolojia ili kuchochea mabadiliko ya kijamii na kuziba pengo la kidijitali.

Kwa mujibu wa Waziri Silaa, jitihada hizi za Serikali kwa kushirikiana na wahisani zinaweka msingi imara wa kuzalisha wataalamu wa TEHAMA wa kutosha, watakaokuwa nguvukazi muhimu ya Taifa kwa siku zijazo.