Habari
WAZIRI SILAA AWASIHI WATUMISHI WA POSTA KUWA WABUNIFU NA WAZALENDO
Na Mwandishi Wetu, WMTH, Dar es Salaam
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb) amewasihi watumishi wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uzalendo, na ubunifu ili kufanikisha maendeleo ya Shirika hilo na taifa kwa ujumla.
Waziri Silaa ametoa wito huo leo tarehe 10 Januari, 2025 wakati akifungua Mkutano wa 31 wa Baraza Kuu la wafanyakazi la Shirika la Posta Tanzania uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Waziri Silaa amewasihi watumishi wa Shirika hilo kuacha utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea. "Kila mtumishi ana wajibu anaopaswa kutekeleza, wote tunafahamu hakuna haki pasipo wajibu, ni vema kila mmoja afanye kazi kwa weledi, uzalendo, na ubunifu," alisema Waziri Silaa.
Aidha, ameitaka TPC kujadili utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2023/24 na utekelezaji wa ahadi zilizotolewa wakati ikiwasilishwa bungeni huku akilipongeza Shirika hilo kwa kuendelea kuwa wabunifu katika utoaji wa huduma, akisema kuwa ubunifu ni njia pekee ya Shirika kufanya vizuri zaidi.
Waziri Silaa amelitaka Shirika kuzingatia sheria katika utekelezaji wa majukumu yao, hasa Sheria mpya ya Manunuzi pamoja na kujitathmini kwa kina na kutekeleza hoja zote za ukaguzi, akisema kuwa hatarajii kuona hati zenye mashaka au zisizoridhisha.
"Mjipange vema, mikakati mnayopendekeza isiwe ya kufikirika, iwe ya uhalisia na inayotoa matokeo tarajiwa. Shirika hili ni la kimkakati, hakikisheni wataalam wa ndani wanatumika kutekeleza majukumu nyeti ya Shirika," alisema Waziri Silaa.
Pia, alielekeza kuwa Watumishi wa Shirika la Posta wapelekwe mafunzo mara kwa mara ili kuongeza tija na ubora katika utendaji kazi wao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi na Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Macrice Mbodo amesema Baraza hilo ni kama "bunge" la Shirika, na kuahidi mbele ya Waziri Silaa kuwa uchaguzi wa wajumbe wa Baraza utakuwa huru, haki, na wazi kwa wajumbe wote kushiriki.
Ameongeza kuwa Baraza la wafanyakazi litakuwa na mwelekeo mmoja na mtazamo wa kuifanya Shirika la Posta kuwa la kidijitali na kuleta biashara endelevu.