Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAZIRI SILAA AFUNGUA KITUO CHA TAARIFA CHA KILIMANJARO TELECOM NCHINI UGANDA


Na Mwandishi Wetu, WMTH, Uganda
 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa, ameanza ziara rasmi ya siku mbili nchini Uganda kufuatia mwaliko wa Waziri wa TEHAMA na Miongozo ya Kitaifa wa Jamhuri ya Uganda, Mhe. Dkt. Chris Baryomunsi.

Katika siku ya kwanza ya ziara yake, tarehe 21 Julai, 2025 Mhe. Silaa amefungua rasmi kituo cha kuhifadhi taarifa (data center) cha Kilimanjaro Telecom Co. Limited kilichopo nchini Uganda. Kituo hiki kitakuwa kiunganishi muhimu kwa huduma za Mkongo wa Taifa, kikihifadhi na kusambaza mawasiliano kwa ajili ya matumizi ya ndani ya Uganda na mataifa jirani.

Katika hatua nyingine, Mhe. Silaa alitembelea Kampuni ya Kilimanjaro Telecom Co. Limited, ambayo ni miongoni mwa wateja wa huduma za intaneti kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, unaosambazwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL).

Mhe. Silaa alipongeza ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda katika kuimarisha miundombinu ya TEHAMA, akisisitiza kuwa “mawasiliano ya uhakika na ushirikiano wa kikanda ndivyo vitakavyowezesha mapinduzi ya kidijitali kwa Afrika.”

Ziara hiyo ya Waziri Silaa nchini Uganda inalenga kuimarisha ushirikiano katika sekta ya TEHAMA baina ya nchi hizi mbili, ikijumuisha maunganisho ya miundombinu ya TEHAMA, soko la kidijitali na matumizi ya teknolojia kwa maendeleo jumuishi.