Habari
WAZIRI NAPE: SERIKALI INAENDELEA KUTATUA NA KUIMARISHA SEKTA YA HABARI NCHINI
Na. Paschal Dotto, WHMTH
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewapongeza wafanyazakazi wa Channel 10 na Magic FM kwa kutangaza kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutatua kero na kuendelea kuimarisha sekta ya Habari nchini.
Waziri Nape ameyasema hayo alipotembelea Vyombo hivyo leo Februari 15, 2023 akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kutembelea vyombo vya Habari na kujionea utendaji kazi wake, Nape amesema kuwa Rais Samia amedhamiria kuimarisha uchumi wa vyombo vya Habari nchini.
“Channel 10 mnafanya kazi nzuri ya kutangaza kwa wananchi mambo mbalimbali yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita Chini ya Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan, kazi kubwa inafanyika na Rais Samia ni Pamoja na kutueleekeza kupitia hali ya uchumi wa vyombo vya Habari na wanahabari wenyewe ili kuwawezesha kuwa huru katika kutekeleza majukumu yao”, Alisema Waziri Nape.
Aidha, Wzairi Nape ameeleza jinsi Serikali inavyokwenda kuimarisha sekta ya Habari kupitia utekelezaji wa mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ambapo kwa mara ya kwanza muswada wake uliwasilishwa Bungeni hivi karibuni.
Nape, alisema kuwa Sheria hiyo inaenda kulinda maslahi ya waandishi wa Habari kwa kuwapa mikataba na vyombo vya Habari ambavyo wanavitumikia, lakini pia itaangalia namna ya kumlinda mwandishi wa Habari baada ya kazi kwa kumpatia bima ya afya ili aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Katika kuimarisha uchumi kwa vyombo vya Habari, Waziri Nape alitekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuunda kamati ambayo itapitia uchumi wa kila chombo cha Habari nchini na kuiwasilisha ambapo Serikali itaifanyia kazi ili kuboresha uchumi wa vyombo vya Habari na wanahabari.
Pia, Waziri Nape alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imefanyikisha kiu ya kila mwananchi ya kuona sekta za Tehama, Habari na Mawasiliano zinaunganishwa na kuwa Wizara moja inayofanya kazi kwa Pamoja kuwaidia wananchi.
“Katika mambo ambayo Serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa ni kuvileta vipande vya Tehama, Habari na Mawasiliano lakini pia kubadilisha utendaji kazi kutoka utendaji kazi wa kukaripiana na kuwa utendaji kazi wa kushirikishwa.
Katika Sekta ya Mawasiliano Waziri Nape alisema kuwa mpaka sasa kwa Tanzania kuna watumiaji wa laini za simu milioni 61 ambapo watumiaji na watumaji hela kupitia matandao wa simu wako milioni 40, kwa hatua nyingine Waziri Nape aliosema kuwa zaidi ya laini za simu laki 9 zimezimwa kufikia jana na kuongeza kuwa Serikali imetoa siku 90 kwa wenye simu ambazo zimezimwa na wanazihitaji wanawezea kuzirudisha ndani ya siku hizo.