Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAZIRI NAPE: MTAKUWA NA UWEZO WA KUIANGALIA DUNIA KUTOKEA MSOMERA


WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, amesema, zoezi la kuboresha huduma za Mawasiliano katika makazi mapya ya wafugaji wa jamii ya Kimasai litawafanya waweze kupata taarifa mbalimbali duniani kupitia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano

Waziri Nape ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa upatikanaji wa huduma za Mawasiliano pamoja na maendeleo ya zoezi la ukusanyaji wa taarifa za Watu na Makazi katika kijiji cha Msomera kilichopo Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga ambako wakazi wapya kutoka Ngorongoro wanaishi.

“Mtakuwa na uwezo wa kuangalia Dunia kutokea Msomera hapa, na sisi kazi yetu ni kuwaunganisheni na Dunia ili mpate hizo huduma na ndiyo maana tumekuja na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), tunataka watoto wenu waanze kujua kuchezea Kompyuta, wajue Dunia inavyoeenda na nina uhakika vijiji vingine vitawaonea wivu Msomera” Waziri Nape

Waziri Nape aliipongeza kampuni ya Airtel Tanzania kwa kupelekea huduma ya Mawasiliano katika kijiji hicho, pia mwisho wa mwezi huu mnara mkubwa unaojengwa na TTCL utakamilika na Wananchi wa kijiji hicho wataweza kupata huduma zote za Mawasilino kutoka mitandao yote nchini.

Sambamba na hayo Waziri Nape ameongeza kuwa Utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi ni jambo endelevu na hivyo aliongozana na wataalam wa Wizara yake ili kuhakikisha Msomera inawekewa mfumo huo ili kurahisisha upatikanaji wa huduma nyingine za kijamii na kuifanya Msomera kuwa Kijiji cha Kidijitali.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Siriel Mchembe ameipongeza kampuni ya Airtel Tanzania kwa kufanya kazi muda wote kufanikisha upatikanaji wa Mawasiliano katika kijiji hicho ambapo awali kulikuwa na shida ya mawasiliano.

Naye, Mwenyekiti wa Kijiji cha Msomera, Bw. Martin Olykei Paraketi amepongeza kwa dhati juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada wanazofanya kuhakikisha Msomera inakuwa na Mawasiliano bora pamoja na huduma nyingine za kijamii.

Serikali imekuwa ikitoa hamasa kwa jamii ya kabila ya Wamasai kuhama kwa hiari kutoka Ngorongoro na kwenda katika Kijiji cha Msomera kilichopo wilaya ya Handeni Mkoani Tanga, ili kutunza mazingira kwani jamii hii asili yao ni ufugaji na kwa miaka ya hivi karibuni imekuwa ikiongezeka kwa kasi na kuongezeka kwao pamoja na   mifungo yao na hivyo kunahatarisha mazingira ya hifadhi ya Loliondo.