Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAZIRI NAPE AWAJULIA HALI MAJERUHI HOSPITALI YA BUGANDO


MWANZA

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amewajulia hali majeruhi wa ajali iliyotokea jana katika Wilaya ya Busega mkoa wa Simiyu.

Waziri Nape alisema kuwa amefarijika kuona majeruhi wanaendelea vizuri mara baada ya kupata matibabu na hata sasa angalau wanaweza kuzungumza kidogo, majeruhi hao ni Tunu Herman na Vanny Charles ambao ni wanahabari.

"Nawapongeza madaktari wa hospitali ya Bugando na watumishi wote wa afya kwa kutoa matibabu mazuri kwa majeruhi  hata sasa kama tulivyowaona angalau wanajitambua, pia nashukuru uongozi wa Mkoa wa Mwanza kwa jitihada mbalimbali walizofanya ili kusaidia majeruhi hawa waweze kupata msaada wa haraka" alisema Waziri Nape

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel alisema kuwa anamshuru Mhe. Waziri kwa kuwatembelea majeruhi na anawapongeza madaktari kwa kufanya jitihada za makusudi za kukoa  maisha yao.

Aidha, ameendelea kuipongeza na kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kununua vifaa vya kisasa ambavyo vimetumika katika kufanya uchunguzi wa majeruhi hao na hivyo imesaidia kutosafirisha majeruhi hao nje ya Mkoa au nje ya nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Rufaa  Bugando Dkt. Fabian Massaga alisema kuwa hali ya majeruhi inaendelea vizuri , madaktari bingwa na matabibu wanaendelea kuwapatia huduma mbalimbali ili afya zao ziendelee kuimarika

Aidha, ametoa rai kwa wadau wa sekta ya usafiri kuweka mikakati ya kupunguza ajali za barabarani kwa kuwa ajali  sio magonjwa yanayoambukiza  hivyo zinaepukika.

Katika Hatua nyingine, Waziri Nape alihudhuria mazishi ya mmoja wa waandishi aliyezikwa leo Husna Milanzi ambapo katika mazishi hayo aliambatana na viongozi  mbalimbali wa Mkoa wa Mwanza pamoja na wana habari