Habari
Waziri Nape Ashiriki Kongamano la Kimataifa la Wadhibiti wa Huduma za Mawasiliano Kampala-Uganda

Waziri wa Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb)akiwa na ujumbe kutoka Tanzania ambao ni Mhandisi Peter Mwasalyanda kutoka Wizarani, Bw. John Daffa Mkurugenzi wa Leseni na Ufuatiliaji pamoja na Mhandisi Mwesigwa Felician Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta wote kutoka TCRA ameshiriki katika Kongamano la Kimataifa la Wadhibiti wa Huduma za Mawasiliano (Global Symposium for Regulators) linalofanyika kuanzia tarehe 1 hadi 4 Julai, 2024, Kampala, Uganda.
Kongamano hilo linaloandaliwa na Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU) ni jukwaa la kimataifa la kujadiliana mbinu bora za kusimamia huduma za mawasiliano.
Mwaka 2024, kongamano hili linajadili masuala ya kiudhibiti yakiwemo ya Satelaiti na Uchumi wake (space economy), mabadiliko ya Kidijiti (digital transformation), Usalama Mtandaoni, Akili Mnemba, Fedha Mtandao, na Miundombinu ya Mawasiliano, kati ya mengine mengi. Kongamano hilo pia litaridhia miongozo bora ya udhibiti ya mwaka 2024.