Habari
Waziri Nape Aridhishwa, Maandalizi ya Kongamano Sekta ya Habari na Kikao Kazi cha Maafisa Habari

Na. Mwandishi Wetu, DSM.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb) leo tarehe 17 Juni, 2024 amekagua maandalizi ya Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari na Kikao Kazi cha 19 cha Maafisa Habari wa Serikali.
Akizungumza baada ya kukagua maandalizi hayo katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam, Mhe. Nape alisema kuwa ameridhishwa na maandalizi hayo.
“Maandalizi ya vikao viwili muhimu vya tasnia ya habari ambapo kikao cha kwanza kitakuwa kikao cha Kongamano la sekta ya habari, ambapo kama mnakumbuka Rais Samia baada ya kuingia madarakani aliagiza tuwe na kongamano la habari kila mwaka ili kufanya tathmini ya sekta ya habari; hivyo nimekuja kufanya ukaguzi wa maandalizi na nimeridhika”, alisema Waziri Nape.
Waziri Nape alisema kuwa kubwa katika Kongamano hilo mgeni rasmi ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan, ambaye atafungua kongamano hilo muhimu nchini.
Aidha, katika kongamano hilo kutakuwa na mijadala mbalimbali ya kitaalam kwa siku mbili ya kesho na kesho kutwa ambapo baada ya mijadala hiyo kwa siku mbili kutakuwa na vikao vya maafisa habari na mawasiliano wa serikali.
Pia, katika kongamano hilo taarifa ya tathmini ya hali ya uchumi wa vyombo vya habari nchini, ikumbukwe kuwa kikosi kazi cha wataalam kiliundwa ili kuangalia suala hilo na kazi imekamilika ambapo kesho utawasilishwa mbele ya Mhe.Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema kuwa baada ya ripoti hiyo kukabidhiwa kwa Mhe. Rais itakuwa hadharani na kujadiliwa, na serikali kuchukua hatua na kuweka mipango ya uwekezaji ambapo itakuwa mpango mzuri wa kubadili hali ya wanahabari nchini.