Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAZIRI NAPE APOKEA UJUMBE WA FINLAND, WAZUNGUMZIA MASHIRIKIANO KATIKA TEHAMA


Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) leo Januari 31, 2023 amepokea ujumbe wa Serikali ya Finland pamoja na watendaji wa makampuni binafsi kutoka Finland ofisini kwake jijini Dodoma. 

Ujumbe huo ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Uchumi wa nchi hiyo Mhe. Mika Lintillå umepokelewa na Waziri Nape akiambatana na Menejimenti ya Wizara hiyo na kufanya mazungumzo kuhusu mashirikiano na kubadilishana uzoefu katika TEHAMA.

“Tumekuwa na mahusiano na mashirikiano ya muda mrefu na nchi ya Finland katika Tehama na kuweza kusaidiana nao katika maeneo mengi. Finland ni nchi ndogo ambayo imepiga hatua kubwa katika masuala ya Tehama”, Amezungumza Waziri Nape

Ameongeza kuwa, “Tumekubaliana Wizara na nchi ya Finland kupitia ubalozi wao nchini tutengeneze maeneo ya mashirikiano zaidi ili kuona namna tunaweza kutumia uzoefu wao pamoja na teknolojia yao lakini pia kuwavutia wawekezaji waje kuwekeza katika eneo la TEHAMA.”