Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAZIRI NAPE ALIAGIZA SHIRIKA LA POSTA KUWA WABUNIFU ILI HUDUMA ZAO ZIWEZE KULETA TIJA KWA WANANCHI


Na WHMTH, Arusha.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) ameliagiza Shirika la Posta Tanzania (POSTA) kuwa wabunifu katika kutangaza shughuli wanazozifanya ili huduma zao ziweze kuleta tija kwa wananchi.

Waziri Nape ameyasema hayo wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Biashara ya Bima ya Shirika la Posta (Posta Insurance Broker) katika ukumbi wa Hoteli ya Mount Meru - Arusha, leo Julai 28, 2023. 

“Kuanzishwa kwa huduma au Biashara ni jambo moja lakini kuwafikia walengwa ndiyo jambo la msingi, hivyo nawaelekeza Posta Ili muweze kufikia malengo, nguvu kubwa inahitajika katika kuitangaza biashara yenu katika vyombo vya habari, na kuwafuata walengwa walipo kupitia njia mbalimbali ikiwemo mikutano na semina mbalimbali ili kuwapa elimu ya umuhimu wa bima hasa wale wakulima wa vijijini ambao ofisi nyingi za Posta ndiko ziliko.” Amesema Waziri Nape

“Kuna baadhi ya huduma nyingine za Posta zitazidi kufahamika kwa jamii kupitia wateja wapya watakaofika katika ofisi za Posta kupata huduma za Bima. Mteja anapofika kupata huduma hiyo atakutana na huduma nyingine zitakazomvutia zaidi “ Amesema Waziri Nape

Katika hatua nyingine Waziri Nape amewapongeza Shirika la Posta kwa Ubunifu waliofanya wa kuanzisha Bima hiyo kwani ni ishara tosha ya kuunga jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha kuwa Watanzania wengi wanapata fursa ya kuunganishwa na mifumo rasmi ya watoa huduma mbalimbali mahali pamoja ili kurahisisha huduma kwa jamii, hivyo kuharakisha ukuaji wa uchumi wa wananchi na taifa hili kwa ujumla.