Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAZIRI MKUU MAJALIWA AZINDUA RUANGWA FM


Na Juma Wange, WHMTH, RUANGWA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb), alizindua Kituo cha Radio Jamii cha Ruagwa Mkoani Lindi mnamo Januari 06, 2024. Katika hafla hiyo, alisisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kuwa wananchi wote wa Tanzania wanapata haki yao ya kikatiba ya kupata habari kama ilivyoainishwa katika ibara 18 (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
 
Majaliwa alirejelea sehemu ya Katiba inayozungumzia haki ya wananchi kupata habari, ikisisitiza kuwa kila raia ana haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi pamoja na masuala muhimu kwa jamii.
 
Aidha, aliongelea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020-2025; Ibara ya 125 (a) ambayo imeielekeza serikali kuendelea kutekeleza Sheria ya Huduma za Habari Na. 12 ya mwaka 2016 ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata taarifa sahihi kwa urahisi zaidi na kwa wakati.
 
Uzinduzi wa kituo hicho cha radio ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Ilani ambayo inalenga kuboresha sekta ya habari kwa kuongeza wigo wa upashanaji wa habari na hivyo kuongeza fursa za wananchi kupata habari.
 
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb), alitoa wito kwa wafanyakazi wa Radio mpya ya Ruangwa FM kutafuta habari katika maeneo yao kwa kwenda mtaani, zikiwemo taarifa za miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.
 
Bi. Justina Mashiba, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), alitangaza azma ya mfuko huo kupeleka huduma ya mawasiliano kote nchini na kuhakikisha kuwa Halmashauri zote 184 zinakuwa na Radio kama hiyo.
 
Kituo hiki cha radio kimejengwa kwa ushirikiano kati ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Nchini (UCSAF).