Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAZIRI MKUU AZINDUA RADIO JAMII KATIKA HALMASHAURI YA MPIMBWE


Na Mwandishi Wetu

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) amewataka  viongozi na wataalamu wa maeneo ambapo kuna Radio Jamii kuzitumia kutatua kero za  Wananchi wa maeneo hayo ili kutimiza ahadi ya serikali ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa wananchi. 

Ameyasema hayo tarehe 25 Februari, 2024 alipohudhuria hafla ya uzinduzi wa Radio Jamii ya Mpimbwe FM iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe, mkoani Katavi.

Mhe. Majaliwa (Mb) ameipongeza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kuendelea  kufungua vituo vya Radio Jamii katika Halmashauri mbalimbali nchini kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Mkurugenzi na Watumishi wote wa Halmashauri ya Mpimbwe kwa kazi kubwa ya usimamizi wa ujenzi wa Radio Jamii katika halmashauri hiyo.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Selestine Gervas Kakele ameeleza kuwa sekta ya mawasiliano imejikita zaidi katika kuimarisha ubora wa Mawasiliano nchini na kuhakikisha wigo wa Mawasiliano unaongezeka na kuwafikia Wananchi wote hivyo basi, kukamilika kwa ujenzi wa studio hizi za Radio Jamii katika Halmashauri ya Mpimbwe ni hatua muhimu katika kuhakikisha kwamba huduma za maudhui ya redio zinapatikana maeneo yote nchini.

Vilevile, ameeleza kuwa ufikishaji wa huduma za maudhui ya redio katika maeneo mbalimbali nchini utachochea maendeleo katika maeneo hayo , hii inatokana na ukweli kwamba huduma za maudhui ni chanzo cha ajira , burudani na upashanaji wa Habari muhimu za kiuchumi na kijamii kwa wananchi watakaofikiwa na mawimbi ya redio hii.

Sambamba na hayo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ( UCSAF), Eng. Albert Richard amesema kutokana na changamoto iliyokuwepo ya usikivu wa Redio ya Taifa kwa baadhi ya maeneo ndani ya nchi yetu hususan maeneo ya miradi ya kimkakati na maeneo ya mipakani mwa nchi yetu, UCSAF kwa kushirikiana na Shirika  la Utangazaji Tanzania (TBC), ilingia mikataba ya kuhakikisha huduma ya matangazo ya Redio inawafikia Wananchi wengi zaidi kwa kujenga na kuboresha miundombinu ya kurushia matangazo na studio za redio ya Taifa katika maeneo mbalimbali ya nchi kuwa ya kisasa. 

Mkoa wa Katavi, UCSAF kwa kushirikiana na TBC wameingia makubaliano  kujenga mnara wa Redio katika Wilaya ya Mlele, utekelezaji wa mradi umekamilika kwa upande wa Halmashauri ya Wilaya Mpimbwe. Serikali kupitia UCSAF kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mpimbwe imetekeleza mradi wa uanzishwaji wa kituo Cha Redio Mpimbwe.