Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAZIRI MKUU AFUNGUA MKUTANO WA TANO WA TEHAMA ULIOWAKUTANISHA WATAALAMU WA TEHAMA PAMOJA NA WADAU ZAIDI YA 800


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Tano wa Mwaka wa TEHAMA jijini Arusha

 

ARUSHA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amefungua Mkutano wa Tano wa Mwaka wa TEHAMA ambapo wataalamu wa TEHAMA zaidi ya 800 wamehudhuria Mkutano huo

Tukio hilo la ufunguzi limefanyika leo tarehe 22 Oktoba, 2021 jijini Arusha katika Ukumbi wa Kimataifa wa AICC ambapo kwa kwaka huu Mkutano huo unaenda na Kauli Mbiu ya “Kujenga Taifa la Kidijitali”

Mhe. Majaliwa amewataka wataalamu wa TEHAMA pamoja na wadau kuainisha changamoto zote zilizopo katika Sekta ya TEHAMA nchini ili Serikali iweze kuzifanyia kazi kwa lengo la kujenga uchumi wa kidijitali nchini

“Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika TEHAMA ambayo ndio nguzo kuu ya kufikia uchumi wa kidijitali ambapo shughuli za kiuchumi, kijamii na uzalishaji zinakwenda kuendeshwa kwa kutumia teknolojia za juu za TEHAMA”, amezungumza Mhe. Majaliwa

Ameongeza kuwa, “Serikali imedhamiria katika kipindi cha miaka mitano ijayo nchi ya Tanzania ionekane kama moja ya nchi ambayo imeleta mageuzi makubwa ya TEHAMA barani Afrika na kwenye ramani ya ulimwengu”

Amesema kuwa ilani ya chama cha mapinduzi ya mwaka 2020-2025 inasema bayana azma ya kukuza uchumi wa kidijitali kwa kutumia teknolojia zilizopo na zile zitakazobuniwa na wabunifu nchini ili kuweza kujenga uchumi wa kidijitali.

Pamoja na mambo mengine Waziri Mkuu ametoa maelekezo kwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutekeleza mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi kwa kasi kubwa ili kurahisisha ufikishaji wa huduma kwa wananchi mpaka nyumbani

Mhe. Majaliwa amesema kuwa Serikali ina dhamira ya kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika TEHAMA ili kukuza ajira na kuongeza mchango wa Sekta ya TEHAMA kwenye pato la Taifa

Aidha amemuelekeza Waziri mwenye dhamana ya TEHAMA pamoja na taasisi zote zilizopo chini yake kuhakikisha kila mwaka Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Kituo cha Uwekezaji (TIC) kinapata taarifa ya mapendekezo ya vivutio vya uwekezaji wa TEHAMA kwa lengo la kutoa hamasa na motisha kwa wawekezaji ili waweze kuwekeza katika TEHAMA  

Katika hatua nyingine Mhe. Majaliwa ameitaka Wizara kuendelea kusimamia upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kuufikisha katika Wilaya zote nchini mpaka kwenye miji midogo ili wananchi wengi zaidi waweze kushiriki katika uchumi wa kidijitali

Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa ametoa maelekezo kwa Wizara kushirikiana na Wizara ya mambo ya Ndani ya nchi ili kuweka mitambo ya ulinzi na usalama kwa kuhakikisha miji mikubwa inafungwa kamera na mifumo ya ulinzi na usalama

Awali, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji  amesema kuwa mkutano huo wa TEHAMA ulihusisha wataalamu wa TEHAMA, wawekezaji, wabunifu, makampuni binafsi wadau na wadhamini wa Mkutano huo ambao ulitarajiwa kuwa na jumla  ya washiriki 600 lakini kutokana na mwitikio chanya washiriki wa Mkutano huo wamekuwa zaidi ya 800

Amesema kuwa Wizara hiyo kupitia Tume ya TEHAMA ilianza utaratibu wa kuwatambua na kuwasajili wataalamu wa TEHAMA mwaka 2019 na zoezi la usajili linaendelea  vizuri ambapo mpaka sasa wataalamu 700 wamesajiliwa na Tume hiyo

Ameongeza kuwa katika kuweka msisitizo wa kuwatambua na kuwasajili wataalamu hao Mwongozo wa usajili wa wataalamu wa TEHAMA Tanzania umeandaliwa na kuzinduliwa rasmi na Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akifungua Mkutano huo leo  tarehe 22 Oktoba, 2021 jijini Arusha

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Mhe. Moshi Kakoso amewapongeza watendaji wa Wizara kwa namna ambavyo Wizara inasimamia vema utekelezaji wa miradi na mipango mbalimbali ya Wizara hiyo katika kuinua Sekta ya TEHAMA na Mawasiliano nchini na kuiomba Serikali kuendelea kuwekeza zaidi katika sekta hiyo kupitia Wizara na taasisi zake

Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA Samson Mwela amesema kuwa Mkutano wa Mwaka wa TEHAMA ulianza kufanyika mwaka 2017 na kwa mwaka huu mbali na wananchi kuona maonesho mbalimbali ya TEHAMA pia kulikuwa na mkutano wa wawekezaji wa TEHAMA na Tuzo za TEHAMA 18 zimetolewa katika maeneo mbalimbali ya matumizi ya TEHAMA kwa mara ya kwanza.