Habari
Waziri Kairuki: Mazingira Bora ya Uwekezaji Yataendelea Kuimarishwa Chini ya Serikali ya Rais Sami
Na Mwandishi Wetu WMTH, Dar es Salaam
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amesema Serikali inaendelea kuimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji ili kuchochea uchumi wa nchi na maendeleo kwa Watanzania.
Mhe. Kairuki ameyasema hayo leo tarehe 12 Desemba, 2025 wakati wa ziara yake ya Kikazi katika Kampuni ya Helios Towers Tanzania inayoshughulika na Ujenzi wa Minara ya Mawasiliano ya Simu.
“Chini ya uongozi wa Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan tunahakikisha tunaboresha mazingira ya uwekezaji, tukilenga kukuza uchumi wa nchi na maendeleo ya wananchi. Tutahakikisha mnapata ushahidi na mazingira mazuri yanayothibitisha uwepo wa soko bora la uwekezaji Tanzania,” amesema Waziri Kairuki.
Akizungumzia mchango wa sekta ya mawasiliano, Waziri Kairuki alisisitiza kuwa sekta hiyo ndiyo injini ya mageuzi ya kiuchumi na kijamii, na kwamba kampuni kama Helios Towers Tanzania zinabeba jukumu muhimu katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali.
“Tuendelee kufanya kazi, tuendelee kushirikiana. Tunajivunia kuona asilimia kubwa ya wafanyakazi wenu ni Watanzania,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Helios Towers Tanzania, Bw. David Dzigba, alimshukuru Waziri Kairuki kwa ziara hiyo akiwa ni Waziri wa Kwanza kutembelea Kampuni hiyo toka ilipoanzishwa.
“Tunaahidi kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha Tanzania inafikia azma yake ya kuwa taifa lenye uchumi wa kidijitali wenye ushindani wa kimataifa,” alisema Bw. Dzigba.
Waziri Kairuki aliongozana na Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb) pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Bw. Nicholaus Merinyo Mkapa na baadhi ya watendaji wa Wizara kwa lengo la kujifunza na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi katika sekta ya Mawasiliano na TEHAMA kwenye ujenzi wa miundombinu imara ya mawasiliano, ambayo ni nyenzo muhimu katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kijamii nchini.
