Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Waziri Kairuki: Huduma Nafuu na Bora ni Kipaumbele kwa Watumiaji wa Mawasiliano


Na Mwandishi Wetu – WMTH, Dar es Salaam

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), ameitaka Halopesa, inayomilikiwa na Halotel, kuendelea kuwekeza katika upanuzi wa huduma zake nchini, hususan katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma za Mawasiliano. 

Waziri Kairuki ametoa wito huo tarehe 11 Desemba, 2025 alipotembelea Makao Makuu ya Kampuni ya Halotel wakati wa ziara yake ya kikazi kutembelea watoa huduma za mawasiliano.

Waziri Kairuki amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka kipaumbele katika kukuza maendeleo ya kidijitali, hivyo Halotel ina wajibu wa kuendeleza uwekezaji unaoendana na dira hiyo.

Aidha, Waziri Kairuki ameitaka Halotel kufuata kikamilifu taratibu, sheria na kanuni za nchi, akisisitiza kuwa kampuni hiyo ikiwa na ushiriki wa Serikali ina jukumu la kulinda maslahi ya Taifa na watumiaji wake.

Akizungumzia umuhimu wa kuongeza uelewa kwa wananchi, Waziri Kairuki amewataka Halotel kuongeza juhudi katika kutoa elimu juu ya matumizi salama na sahihi ya teknolojia za kidijitali pamoja na kuendeleza kampeni yao ya Fiber to the Home pamoja na kuongeza kasi ya uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano, ikiwemo huduma za 4G na 5G.

Waziri Kairuki amewahakikishia uongozi wa Halotel kuwa Serikali itaendelea kuandaa mazingira wezeshi na rafiki ya biashara ili kuongeza uwekezaji nchini na kuhakikisha kampuni zinafaidika sambamba na wananchi.

Akiwapongeza kwa kutimiza miaka 10 ya uwekezaji nchini, Waziri Kairuki ameitambua Halotel kwa mchango wake mkubwa katika kukuza uchumi kupitia uwekezaji na huduma za mawasiliano. Amewahimiza kuongeza juhudi zaidi katika kupanua huduma, hasa vijijini, ili kuharakisha mapinduzi ya kidijitali.

Waziri Kairuki ameipongeza Kampuni ya Halotel kwa kuchangia takribani shilingi bilioni 900.2 kupitia mifumo ya kodi na tozo mbalimbali, pamoja na dhamira ya kuwekeza dola bilioni moja kwa ajili ya kupanua huduma na miundombinu ya mawasiliano nchini.