Habari
Waziri Kairuki Azungumza na Mtendaji Mkuu wa EACO Kuhusu Tafiti za Mawasiliano za EAC
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amefanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Mawasiliano la Afrika Mashariki (EACO,), Bi. Caroline Koech, pembezoni mwa Hafla ya Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi tarehe 8 Februari 2026.
Katika kikao hicho, Bi. Koech alieleza majukumu ya taasisi hiyo, ikiwemo kufanya tafiti mbalimbali katika Sekta ya Mawasiliano zinazolenga kutafutia ufumbuzi wa changamoto zilizopo katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Miongoni mwa tafiti hizo ni pamoja na njia za kupunguza changamoto kwa wananchi wanaoishi mipakani, ambao hupata mawasiliano nje ya nchi zao bila ridhaa yao (forced roaming), hali inayoongeza gharama za mawasiliano katika maeneo hayo.
Waziri Kairuki alipongeza jitihada za taasisi hiyo, ikiwemo ushirikiano na Mamlaka za Mawasiliano na watoa huduma wa mawasiliano wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na aliihimiza kuendeleza tafiti zinazolenga kutatua changamoto husika.
