Habari
Waziri Kairuki Atembelea Ukumbi wa Maonesho wa Teknolojia za Kisasa nchini China
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), ametembelea Ukumbi wa Maonesho wa Von Neumann, unaomilikiwa na Kampuni ya HUAWEI ambapo alijionea teknolojia mbalimbali zinazobuniwa na kutengenezwa na kampuni hiyo uliopo katika jiji la Shenzhen, China.
Katika ziara hiyo, Waziri Kairuki alipata nafasi ya kuona teknolojia za kisasa, ikiwemo miundombinu ya mawasiliano ya simu, mitandao ya kasi ikiwemo 5G, mifumo ya Akili Bandia (Artificial Intelligence), na huduma za wingu (cloud computing), zinavyotumika katika sekta mbalimbali ikiwemo madini, usafiri wa anga, bandari, elimu, afya, huduma za kifedha za simu za mkononi pamoja na suluhu za bunifu za miji janja (smart cities).
Akizungumza na Viongozi wa Kampuni hiyo, Waziri Kairuki aliishukuru Kampuni ya HUAWEI kwa ushirikiano wa zaidi ya Miaka 10 uliopo katika Tanzania na Kampuni hiyo na kuiomba kuendeleza ushirikiano huo kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo katika TEHAMA, ikiwemo ujumuishaji wa kidijitali kupitia upanuzi wa miundombinu ya mawasiliano ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, ujenzi wa minara ya mawasiliano vijijini, pamoja na miradi ya uwajibikaji wa kijamii (CSR).
Aliongeza kuwa lengo la ushirikiano huu ni kuongeza uwezo wa Tanzania katika utoaji wa huduma za umma kupitia teknolojia za kisasa na kuimarisha uchumi wa kidijitali .
Aidha, Waziri Kairuki ameialika Kampuni ya Huawei kuendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo ya kimkakati ikiwemo: ujenzi wa vituo vya mafunzo, maabara za kompyuta zenye mtandao wa intaneti wenye kasi katika shule, upanuzi wa huduma ya Wi-Fi salama katika maeneo ya umma, na usaidizi katika kukuza kampuni changa kwa kuboresha miundombinu ya kidijitali ya kiwango cha biashara.
Maeneo mengine ni kuanzisha “sandbox” kwa ajili ya majaribio ya teknolojia mpya, pamoja na kusaidia utekelezaji wa miji janja kwa kutumia teknolojia za kisasa kama roboti na mifumo ya akili unde.
Ziara ya Kikazi ya Waziri Kairuki ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Tanzania za kukuza sekta ya TEHAMA na kuhakikisha nchi inaimarika kiujuzi na ubunifu, kuharakisha maendeleo endelevu ya uchumi wa kidijitali, huku pia ikihamasisha ushirikiano na sekta binafsi na wadau wa kimataifa.
