Habari
Waziri Kairuki Ataka Kuimarishwa kwa Miundombinu na Huduma za Mawasiliano
Na Mwandishi wetu WMTH,Dar es Salaam.
Mhe. Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na teknolojia ya Habari Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki(Mb), ameitaka Kampuni ya Minara Tanzania
kuendelea kufikisha huduma za mawasiliano katika maeneo ambayo hayajafikiwa ipasavyo, hususan pembezoni mwa miji na vijijini, ili kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma bora za mawasiliano.
Waziri Kairuki ametoa wito huo tarehe 12 Disemba 2025 wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kampuni ya Minara Tanzania huku akihimiza kampuni hiyo
kuendeleza uwekezaji, kuboresha minara na kuimarisha miundombinu ya mawasiliano.
Mhe. Kairuki ameipongeza Minara Tanzania kwa uwekezaji mkubwa walioufanya katika kipindi cha miaka minne tangu kuanzishwa kwake pamoja na kutoa ajira ambapo asilimia 25 ya ajira zimeenda kwa wazawa. Na kuweza kuratibu minara ya Mawasiliano ya simu 1,888 kwa muda mfupi nchini Tanzania na kuchangia pato la nchi kupitia vyanzo mbalimbali.
Mhe. Kairuki amewahakikishia wawekezaji kuwa wamefanya maamuzi sahihi kufanya uwekezaji huo nchini Tanzania na Serikali itaendelea kutoa ushirikiano huku ikihimiza Watoa Huduma za Mawasiliano katika matumizi ya pamoja ya minara ili kupunguza gharama za uendeshaji kwa watoa huduma hao na kuleta urahisi wa gharama kwa watumiaji wa huduma.
"Ninauona mustakabali mzuri na wenye matumaini kwa Kampuni ya Minara Tanzania katika sekta ya mawasiliano nchini, “ alisema Mhe. Kairuki.
Katika upande wa Wajibu kwa Jamii (CSR), Mhe. Kairuki ameitaka Minara Tanzania kubuni na kutekeleza programu mbalimbali za kijamii zitakazosaidia kujenga mahusiano mazuri na jamii zinazozunguka maeneo ya uwekezaji wao, ambayo itajenga taswira nzuri kwa wananchi pamoja na ushirikiano mzuri kati ya wananchi na wao.
Aidha, amesisitiza kuimarisha ufuatiliaji na ulinzi wa miundombinu ili kupunguza matukio ya uharibifu na kuendelea kuhakikisha kuna utendaji bora na kuendelea kulinda usalama wa wafanyakazi yao na minara yao.
