Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Waziri Kairuki Asisitiza Ruzuku ya Mawasiliano Kuelekezwa Maeneo Sahihi


Na Mwandishi Wetu, WMTH – Dodoma

 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amesema Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) una jukumu kubwa la kutekeleza Sera ya TEHAMA, Sera ya Posta na Utangazaji pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, sambamba na Mkakati wa Miaka 10 wa Uchumi wa Kidijitali.

Akizungumza tarehe 15 Disemba, 2025 jijini Dodoma, wakati wa ziara yake katika taasisi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Waziri Kairuki amesisitiza umuhimu wa kuendelea kusimamia malengo sita ya Mfuko huo ili kuhakikisha maeneo ya mijini na vijijini yanapata mawasiliano ya uhakika, huku mifumo ya utoaji huduma ikiboreshwa ili kuwa rahisi, yenye ufanisi na inayoendana na ushindani wa soko.

Aidha, ameitaka UCSAF kuendelea kubaini maeneo yanayohitaji kunufaika na ruzuku ya Serikali, ikiwemo jamii za pembezoni, shule na vituo vya huduma za kijamii, kupitia miradi ya tiba mtandao, kilimo mtandao na biashara mtandao, ili kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Waziri Kairuki ameagiza pia kuwekwa kwa vigezo sahihi vya utoaji wa ruzuku kwa watoa huduma za mawasiliano, hususan katika maeneo yaliyolengwa, ili kuhakikisha ruzuku hiyo inaelekezwa katika maeneo yenye uhitaji mkubwa na kuepusha kupelekwa sehemu ambazo hazina uhitaji wa kipaumbele.

“Tuendelee kujikita katika kuboresha huduma za mawasiliano ya simu, usikivu wa redio, pamoja na kutathmini redio za kijamii zinazopata ruzuku ya Serikali ili kuhakikisha zinafanya kazi kwa mujibu wa malengo yaliyokusudiwa,” amesema Waziri Kairuki.

Ameongeza kuwa UCSAF inapaswa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi iliyopo, kubuni miradi mipya, pamoja na kushirikiana na wadau walio tayari kuendeleza huduma za mawasiliano kwa wote. Waziri Kairuki amehitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa kushughulikia kwa wakati changamoto zinazosababisha kuchelewa kwa utekelezaji wa miradi, ili kuongeza kasi na ufanisi wa utoaji wa huduma za mawasiliano nchini.