Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Waziri Kairuki aagiza kuimarisha kwa fursa na ubunifu wa TEHAMA nchini.


Na Mwandishi Wetu – WMTH, Dar es Salaam

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), ameitaka Kampuni ya Airtel Tanzania kuendelea kutengeneza fursa kwa jamii na kutoa mchango zaidi kwa watu wasiojiweza, akisisitiza kwamba mafanikio makubwa wanayoyapata yametokana na wananchi.

Waziri Kairuki aliyasema hayo tarehe 10 Desemba, 2025 alipotembelea Makao Makuu ya Kampuni ya Airtel Tanzania ambapo aliwapongeza kwa kuwa kampuni ya pili kwa ukubwa katika huduma ya miamala ya kifedha nchini. huku akibainisha kuwa kampuni za mawasiliano zimekuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa.

Aidha, Mhe. Kairuki ameipongeza Airtel kwa kulipa kodi ya takribani trilioni 1.9 katika kipindi cha miaka minne, na hivyo kuchangia maendeleo ya nchi, pamoja na kulipa gawio la takribani bilioni 226 kwa Serikali, ambapo bilioni 118 zimetokana na miamala ya kifedha. Vilevile, ameishukuru kampuni hiyo kwa kutoa ajira 2,187 kwa Watanzania, hatua ambayo inaendelea kuimarisha ustawi wa kiuchumi wa wananchi.

Ameisisitiza kampuni hiyo kuendelea kuboresha huduma za mawasiliano mijini na vijijini, akitaja umuhimu wa kuhakikisha hakuna pengo katika upatikanaji wa vifaa na huduma za kidijitali. Waziri Kairuki amesema kuwa huduma bora, za haraka na nafuu zitachochea zaidi ujumuishaji wa wananchi kwenye uchumi wa kidijitali.

Kadhalika, Waziri ameitaka Airtel kuimarisha programu za uwajibikaji kwa jamii (CSR), akieleza kuwa wananchi ndio watumiaji wakuu wa huduma zao. Ameihakikishia kampuni hiyo kuwa changamoto walizowasilisha zimepokelewa na serikali, na itaendelea kuzifanyia kazi ili kuwezesha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Katika hotuba yake, Waziri Kairuki alisema:
“Tuendelee kujifunza changamoto mbalimbali mnazokutana nazo ili kuhakikisha mnatoa huduma bora kwa wananchi wa mijini na vijijini, na kuhakikisha hakuna anayesalia nyuma katika maendeleo ya kidijitali.”

Waziri Kairuki ameongeza kuwa zipo baadhi ya changamoto na maboresho yanayohitajika katika maeneo ya uwekezaji, kodi na sera, na akawahakikishia kuwa Serikali itayafanyia kazi kwa wakati ili kuwezesha mazingira bora ya uendeshaji wa kampuni hiyo na sekta nzima ya mawasiliano.