Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Waziri Kairuki Apongeza Uwekezaji wa TowerCo of Africa :Atoa Wito wa Kuendelea Kukuza Sekta ya Mawasiliano.


Na Mwandishi Wetu, WMTH–Dar es Salaam

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), ameipongeza Kampuni ya TowerCo of Africa kwa uwekezaji mkubwa waliofanya nchini ndani ya kipindi cha miaka miwili tangu walipoanza shughuli zao Tanzania, ambapo zaidi ya dola za Kimarekani milioni 100 tayari zimewekeza katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya mawasiliano.

Waziri Kairuki ametoa pongezi hizo tarehe 12 Desemba, 2025 alipotembelea ofisi za Kampuni hiyo na kusema kuwa Serikali inathamini mchango wa kampuni hiyo katika kuongeza mapato ya Serikali, ambayo yamewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara na uboreshaji wa huduma za jamii.

“Ninawashukuru sana kwa kazi kubwa mnayoifanya pamoja na uwekezaji wenu. Katika kipindi kifupi mmeonesha dhamira ya dhati ya kuunga mkono maendeleo ya sekta ya mawasiliano nchini,” amesema Waziri Kairuki.

Aidha, Waziri Kairuki ameipongeza kampuni hiyo kwa mchango wake katika uundaji wa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa Watanzania, na kuitaka kuendelea kutoa mafunzo kwa watumishi na wataalamu wake ili kuongeza ufanisi, utaalam na ubora wa rasilimali watu.

“Kama Serikali, tunashukuru kwa mchango wenu katika mapato ya nchi ambayo yanasaidia kugharamia miradi ya maendeleo. Huu ni ushirikiano wenye faida kwa pande zote,” ameongeza.

Waziri Kairuki amewakaribisha viongozi wa TowerCo of Africa kuwasiliana mapema na Serikali pale wanapokumbana na changamoto zozote za kiutendaji katika utekelezaji wa miradi yao, ili ziweze kutatuliwa kwa wakati.

Vilevile, ameitaka kampuni hiyo kuendelea kutumia nishati safi katika uwekezaji wake na kuzingatia utunzaji wa mazingira kama sehemu ya juhudi za pamoja za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Tunawashukuru kwa kazi nzuri mnayoifanya, na tunaamini kupitia nyinyi huduma za mawasiliano zitapatikana kwa ubora wa hali ya juu, zitakuwa salama, nafuu na himilivu bila kumuacha Mtanzania yeyote nyuma,” amehitimisha Waziri Kairuki.

Ziara hiyo inaakisi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na kukuza uchumi wa kidijitali nchini.