Habari
WAZIRI KAIRUKI AMPONGEZA MBUNIFU WA APLIKESHENI YA KUNUNUA BIDHAA MTANDAONI
Na Mwandishi Wetu, WMTH – Arusha
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), alitembelea kampuni changa ya TEHAMA (Startup) ya Westerwelle Startups Haus Arusha kwa lengo la kujionea bunifu mbalimbali za vijana na kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili ili ziweze kukua na kuchangia maendeleo ya sekta ya TEHAMA nchini.
Akiwa katika ziara hiyo, Waziri Kairuki alikutana na mbunifu wa aplikeshini ya Bhaba, ambayo ni jukwaa la biashara mtandaoni (e-commerce) linalowaunganisha wauzaji na wanunuzi kwa urahisi kupitia simu za mkononi.
Waziri Kairuki alimpongeza mbunifu huyo kwa ubunifu na mchango wake katika kuwawezesha wajasiriamali, hususan biashara ndogo na za kati (SMEs), kutumia teknolojia kufikia masoko mapana zaidi ndani na nje ya maeneo yao.
Mkurugenzi wa Bhaba, Bw. Agrey Agustino Mbwana, alimweleza Waziri Kairuki kuwa Bhaba ni app inayowawezesha wauzaji kuorodhesha bidhaa zao kwa kuweka bei, picha na maelezo, huku wanunuzi wakiweza kutafuta, kuangalia na kununua bidhaa mbalimbali kwa urahisi.
Alisema jukwaa hilo linasaidia wafanyabiashara kupata wateja wengi zaidi na kukuza mauzo yao kupitia matumizi ya teknolojia ya kidijitali.
Bhaba inalenga zaidi kuwahudumia wauzaji ambao ni biashara ndogo, maduka na watu binafsi wanaotaka kuuza bidhaa zao mtandaoni, pamoja na wanunuzi wanaohitaji kununua bidhaa mbalimbali kwa urahisi bila kikwazo cha umbali. Aplikeshini hiyo inapatikana bure kwenye Google Play Store kwa watumiaji wa simu za Android.
Ziara ya Waziri Kairuki katika Kampuni Changa ya Westerwelle ya jijini Arusha imeunga mkono dhamira ya Serikali ya kuendeleza bunifu za vijana, kukuza uchumi wa kidijitali na kuimarisha sekta ya TEHAMA ili ichangie kwa kiasi kikubwa maendeleo ya Taifa.
