Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAZIRI KAIRUKI AKABIDHI VIFAA VYA TEHAMA KWA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA


Na Mwandishi Wetu, WMTH, Dodoma

 

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), leo Disemba 15, 2025 amekabidhi vifaa vya TEHAMA kwa Wizara ya Katiba na Sheria na Taasisi zake katika hafla iliyofanyika kwenye Ofisi za Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari zilizopo Mtumba, Jijini Dodoma.

 

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Kairuki amesema kuwa kukabidhiwa kwa vifaa hivyo ni hatua muhimu katika kuimarisha mifumo ya kidijitali ndani ya Wizara ya Katiba na Sheria, jambo litakalosaidia kuongeza ufanisi, uwazi na kasi katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku. Amesisitiza kuwa TEHAMA ni nyenzo muhimu katika mageuzi ya kiutendaji Serikalini.

 

“Tumeshuhudia mapinduzi makubwa katika Taasisi zinazohusika na utoaji wa haki baada ya kuanza kutumika kwa TEHAMA katika Mahakama na Mabaraza kwani tumeshuhudia mashauri mengi kwa sasa yakiendeshwa kwa uharaka na kwa ufanisi, alisema Mhe. Kairuki.

 

Aidha, aliongeza kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kuwekeza katika miundombinu ya TEHAMA ili kuhakikisha Wizara na Taasisi za Serikali zinatumia Teknolojia kwa tija, hususan katika kuboresha mifumo ya utoaji huduma kwa Wananchi.

 

“Mageuzi haya hayalengi teknolojia pekee, bali ni mageuzi ya kiutawala na kiutendaji yanayolenga kuongeza ufanisi, uwajibikaji, uwazi, na utoaji wa huduma bora kwa wananchi”, aliongeza Mhe. Kairuki.

 

Akitoa maelezo ya utangulizi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla alisema kuwa Wizara pamoja na majukumu mengine inatekeleza Mradi wa Tanzania ya Kidijitali ambapo pamoja na masuala mengine kupitia mradi huo, Wizara inaratibu ujengwaji, uunganishaji wa mifumo ya TEHAMA lakini pia kujenga uwezo Taasisi mbalimbali kwa kutoa mafunzo na kuwezesha upatikanaji wa Vifaa mbalimbali vya TEHAMA.

 

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Eliakim Maswi, ametoa shukrani kwa msaada huo ni chachu muhimu katika kuharakisha maendeleo ya TEHAMA ndani ya Wizara na taasisi zake. Na kuongeza kuwa vifaa hivyo vitasaidia kwa kuongeza kiasi katika utekelezaji wa mifumo mbalimbali ikiwemo e-Justice, e-Registry, mifumo ya kuhifadhi kumbukumbu na mifumo mingine ya kidijitali inayolenga kuboresha utoaji wa haki na huduma za kisheria.

 

Jumla ya kompyuta mpakato 70 pamoja na mashine mbili kubwa za kuchapisha (heavy duty printers) zimekabidhiwa kwa Wizara ya Katiba na Sheria, na Taasisi zake vifaa ambavyo vitasaidia kuimarisha uwezo wa watumishi kutumia mifumo ya kidijitali katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.