Habari
Waziri Kairuki Aitaka TCRA Kuboresha Huduma na Kuendana na Kasi ya Maendeleo ya Teknolojia ya Mawasiliano
Na Mwandishi Wetu, WMTH, Dar es Salaam
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), ameielekeza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufanya mapitio ya huduma zake na kupendekeza maboresho yatakayokidhi kasi ya maendeleo ya teknolojia, ikiwemo matumizi ya Teknolojia ya Akili Unde.
Akizungumza na menejimenti ya TCRA tarehe 25 Novemba, 2025, Waziri Kairuki alisema ni muhimu mamlaka hiyo kuzingatia sheria, kanuni na miongozo katika kusimamia sekta ya mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na za viwango.
Aidha, Waziri Kairuki alisisitiza umuhimu wa kuongeza ubunifu, uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu kwa watendaji wa TCRA, huku akibainisha kuwa sekta ya mawasiliano ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa kidijitali nchini. Na kutoa wito kwa taasisi hiyo kuimarisha mafunzo kwa wataalamu wake ili kuongeza ujuzi na uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya kasi ya teknolojia.
Katika ziara yake ya kwanza kwa taasisi zilizo chini ya wizara, Waziri Kairuki aliambatana na Naibu Waziri, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb), Naibu Katibu Mkuu Bw. Nicholaus Merinyo Mkapa, pamoja na baadhi ya wakurugenzi wa wizara. ambapo alipokea taarifa kuhusu utendaji kazi wa TCRA na baadaye kutembelea baadhi ya maeneo ya Taasisi hiyo ikiwemo Maabara ya Tathmini na Uidhinishaji wa Vifaa vya Kielektroniki (Type Approval Laboratory).
Waziri Kairuki aliipongeza menejimenti ya TCRA kwa usimamizi bora wa sekta ya mawasiliano, huku akihimiza kuongezwa kwa utafiti na uhakiki wa aina na kiwango cha ujuzi kwenye bunifu mbalimbali ili kubaini maendeleo na changamoto zinazoikabili sekta hiyo. Alisisitiza kuwa taarifa sahihi za ujuzi na teknolojia ni msingi muhimu wa kupanga maboresho na sera zinazolenga kuendeleza sekta.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabiri Bakari Kuwe, alimshukuru Waziri Kairuki kwa kufanya ziara hiyo na kuahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa. Na kuongeza kuwa TCRA itaendelea kushirikiana kwa karibu na wizara katika kuhakikisha sekta ya mawasiliano inakua na kunufaisha wananchi na taifa kwa ujumla.
