Habari
WAZIRI KAIRUKI AFUNGUA MAFUNZO YA TEHAMA KWA WALIMU WA SHULE ZA SEKONDARI NCHINI
Na Mwandishi Wetu, WMTH – Dar es Salaam
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb.), amefungua rasmi mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa walimu wa shule za sekondari nchini. Mafunzo hayo yanalenga kuwaongezea walimu ujuzi na uwezo wa kutumia teknolojia katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Mafunzo hayo yanaendeshwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kushirikiana na wadau wa sekta za elimu na TEHAMA. Ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa elimu na kuwawezesha walimu kwenda sambamba na mabadiliko ya kasi katika ulimwengu wa kidijitali.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mhe. Kairuki amesisitiza umuhimu wa kuwajengea walimu uwezo wa kutumia TEHAMA kwa ufanisi. Ameeleza kuwa walimu ni nguzo muhimu katika kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya dunia ya sasa, ambayo kwa kiasi kikubwa inategemea teknolojia.
Aidha, mafunzo hayo yanawahusisha walimu kutoka makundi maalumu. Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa matumizi ya TEHAMA katika elimu yanakuwa jumuishi na yanazingatia mahitaji mbalimbali ya walimu na wanafunzi, hivyo kukuza fursa sawa katika matumizi ya teknolojia na upatikanaji wa elimu bora.
Kupitia UCSAF, Serikali itaendelea kujenga uwezo wa walimu na kuimarisha mazingira wezeshi ya matumizi ya TEHAMA katika shule za sekondari nchini. Lengo ni kuifanya teknolojia kuwa sehemu muhimu ya mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji, na hatimaye kuchangia katika ujenzi wa Taifa lenye ujuzi wa kidijitali.
