Habari
Waziri Kairuki Aahidi Kuweka Kasi Mpya Katika Kuimarisha Sekta ya Mawasiliano na TEHAMA
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumteua kuongoza wizara hiyo, akisema kuwa uteuzi huo ni heshima kubwa na fursa ya kuendelea kulitumikia Taifa. Waziri Kairuki aliyasema hayo mara baada ya kuwasili katika ofisi za wizara Mtumba jijini Dodoma, ambako alisisitiza kuwa hii ni wizara ya nane anayopewa dhamana ya kuihudumia katika safari yake ya utumishi wa umma.
Akiwa katika kikao na menejimenti ya wizara, Waziri Kairuki aliwataka watumishi kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia utaalamu wao ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya wizara. Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuendelea kutafuta na kubuni mbinu za haraka, za kisasa na zenye tija katika kudhibiti changamoto mbalimbali za sekta ya mawasiliano na TEHAMA, ikiwemo kupambana na ujumbe wa utapeli mtandaoni na vitendo vingine vya uhalifu wa kimtandao. Aliongeza kuwa hatua madhubuti zinahitajika katika kuhakikisha mifumo ya Serikali inasomana na kufanya kazi kwa ufanisi.
Waziri Kairuki pia alieleza kuwa yuko tayari kujifunza kwa kina shughuli zote za wizara, na atafanya ziara katika kila kitengo pamoja na Taasisi zilizo chini ya wizara ili kujionea hali halisi ya utekelezaji wa majukumu na miradi inayoendelea.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb), alisema wametwaa dhamana hiyo kwa unyenyekevu na wako tayari kushirikiana kikamilifu na wataalamu wa wizara katika kuimarisha sekta ya TEHAMA nchini, hususan katika kusukuma mbele miradi na programu za kisera.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Mohammed Khamis Abdulla, kwa niaba ya menejimenti, aliwahakikishia Waziri na Naibu Waziri ushirikiano wa hali ya juu. Aliahidi kuwa menejimenti itasimamia kikamilifu utekelezaji wa maelekezo yao, kuimarisha uwajibikaji, na kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya TEHAMA ili kuiwezesha Serikali kufikia malengo yake ya kuboresha mazingira ya TEHAMA na kukuza uchumi wa kidijitali nchini.
