Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAZIRI KAIRUKI AAGIZA MABORESHO YA HUDUMA ZA MAWASILIANO ZANZIBAR.


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), tarehe 26 Januari 2026, amefanya ziara ya kikazi Zanzibar kwa lengo la kukagua hali ya upatikanaji wa huduma za Mawasiliano katika visiwa vya Unguja na Pemba.

 Ameeleza kuwa, huduma za simu, intaneti na posta kwa ujumla zimefikia viwango vya kikanuni, ingawa bado kuna changamoto katika baadhi ya shehia na visiwa vidogo. Kufuatia hali hiyo, ameagiza watoa huduma kukaa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania -TCRA  katika kila shehia ili kubaini changamoto na kuzitatua kwa haraka.

Mhe. Kairuki amesisitiza umuhimu wa ukaguzi wa mara kwa mara na kuimarisha ushirikiano kati ya TCRA na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote -UCSAF ili maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara yaweze kupata ruzuku ya ujenzi wa Minara ya Mawasiliano.

Kwa upande wa Shirika la Posta Tanzania, Waziri Kairuki alieleza kuridhishwa na mfumo wa Modern Agencies (Franchises) na kuagiza huduma za EMS na ubadilishaji fedha kuimarishwa ili ziendane na mahitaji ya wananchi.

Katika ziara hiyo, pia Waziri Kairuki alipokea taarifa ya ujenzi wa Telecentres 11 na kuunganishwa kwa shule 77 na huduma za intaneti Zanzibar, huku akiagiza mchakato wa kutafuta viwanja kwa ajili ya ofisi za kanda kuanza mara moja.

Akihitimisha ziara yake, Waziri Kairuki amesema Serikali itaendelea kuhakikisha huduma za mawasiliano zinafika katika kila kona ya nchi kwa lengo la kukuza uchumi wa kidijitali na maendeleo ya Wananchi.