Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAWEKEZAJI SEKTA YA MAWASILIANO KUENDELEA KUUNNGWA MKONO


WHMTH-Dar es Salaam

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye (Mb) amesema Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wawekezaji katika sekta ya mawasiliano ambao wanaleta mageuzi.

Waziri Nape amesema hayo jijini Dar es Salaam alipotembelea kituo cha mkongo wa mawasiliano cha 2 Afrika kinachosimamiwa na Kampuni ya Airtel ambapo kukamilika kwake kutawezesha kuunganisha nchi zaidi ya 30 Afrika.

"Kwanza niwapongeze Airtel kwa kuliona hili ambalo litaleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya Mawasiliano, mkongo huu utakuwa wenye kasi zaidi na utasaidia kuunganisha watu kwa mataifa tofauti, hivyo naamini utatatua kwa kiwango kikubwa changamoto za kimawasiliano"- amesema Waziri Nape.

Waziri Nape ameongeza kuwa kuongezeka kwa mkongo uliopita chini ya Bahari ni dalili nzuri kwani watoa huduma kama vile mitandao ya simu watakuwa na nafasi ya kufanya machaguo juu ya mkongo upi utumike kitu ambacho kinaweza kuchangia kushuka kwa gharama na kuongezeka kwa ubora wa huduma za Intaneti.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Airtel Dinesh Balsingh amesema mkongo huo utakuwa mkombozi na utaleta mageuzi makubwa katika sekta ya mawasiliano.

"Tunaendelea kushirikiana na serikali katika kuhakikisha mwananchi anapata unafuu katika mawasiliano, hivyo kampuni zote za mawasiliano zinaweza kutumia mkongo huu ili tuzidi kumpunguzia gharama mwananchi"-amesema Dinesh.