Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WATUMISHI WHMTH WAKUMBUSHWA UMUHIMU WA USHIRIKIANO KATIKA UTUMISHI WA UMMA


WHMTH, Dodoma

Watumishi wa Wizara ya Habari, mawasiliano na Teknolojia ya Habari wamekumbushwa umuhimu wa kufanya kazi kwa ushirikiano, weledi na upendo ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi

Hayo yamezungumzwa na Bi. Teddy Njau aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Utumishi na Utawala wa Wizara hiyo ambaye amehamishiwa Wizara ya Maji wakati wa hafla fupi ya makabidhiano ya Ofisi hiyo na Bi. Salome Kessy, Mkurugenzi mpya wa Idara hiyo yaliyofanyika leo Machi 10,2023 jijini Dodoma.

Bi. Njau amewaasa watumishi kuzitendea haki nafasi wanazotumikia katika utumishi wa umma kwa kufanya kazi kwa weledi na kushirikiana ili kutekeleza majukumu ya Wizara kwa ufanisi.

“Kila mmoja wetu ni muhimu na anahitajika kwa taaluma yake, hivyo nafasi unayoitumikia sio kwa bahati mbaya bali tunahitajika ili kusukuma gurudumu la maendeleo”, amesisitiza Bi. Njau

Aidha amewashukuru watumishi wa Wizara hiyo kwa ushirikiano mkubwa kwa kipindi chote alichohudumu katika Wizara hiyo na kuwakaribisha katika Wizara ya Maji aliyohamishiwa.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Utumishi na Rasilimaliwatu Bi. Salome Kessy amekabidhiwa rasmi ofisi hiyo na kusisitiza ushirikiano na upendo baina ya watumishi katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara.

Awali akizungumza kabla ya makabidhiano hayo, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Armon MackAchayo amemshukuru Bi. Teddy Njau kwa ushirikiano alioutoa wakati akitumikia katika Wizara hiyo na kumuahidi ushirikiano Bi. Salome Kessy katika kutekeleza majukumu ya Wizara na kuitumikia nchi kwa weledi na ufanisi.