Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WATUMISHI WATAKIWA KUTUNZA SIRI NA NYARAKA ZA OFISI


Na Mwandishi Wetu, WMTH, Arusha.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara hiyo, Bw. Mohammed Khamis Abdulla amewataka watumishi wa Wizara hiyo kutunza siri na nyaraka za Serikali kwa maslahi mapana ya Taifa.

Akizungumza wakati wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo,lililofanyika Februari 18, 2025 jijini Arusha, Bw. Abdulla amesisitiza kuwa ni kosa kisheria kwa mtumishi wa umma kuvujisha nyaraka za ofisi kwa mtu yeyote asiyehusika au kuchapisha mtandaoni bali wanapaswa kufuata utaratibu wa ofisi iwapo kuna jambo linalohitaji ufuatiliaji.

Fauka ya hilo, Bw. Abdulla amewataka watumishi wa Wizara hiyo kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia ya kidijitali kwa kufanya kazi kwa bidii, kuwa wabunifu na wazalendo katika kulitumikia Taifa na kujenga Uchumi wa kidijitali.

Aidha, ameielekeza Idara ya Utawala na Rasilimaliwatu ya Wizara hiyo, kuhakikisha watumishi wa Wizara hiyo wanashiriki kikamilifu kwenye matukio ya Kitaifa akitolea mfano Siku ya wafanyakazi (Mei Mosi), Siku ya Wanawake Duniani ( tarehe 8 ya mwezi Machi) kwa kufanya maandalizi ya ushiriki mapema.

Bw. Abdulla ameongeza kuwa, Ofisi yake ipo wazi kusikiliza watumishi na kufanyia kazi hoja zao bila ubaguzi wa aina yeyote huku akiwasihi watumishi kupendana kwa kutambua kuwa kila mmoja ni zawadi kwa mwenzie. 

Naye Mwakilishi kutoka TUGHE Taifa, Bw. Maulid Kibeneku amewataka wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kuwa huru kuhoji na kutoa mchango wao wakati wa Mikutano ya Baraza la wafanyakazi kwa lengo la kuboresha mazingira ya utendaji kazi.