Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WATUMISHI WA WIZARA YA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI WASHIRIKI SHEREHE ZA MUUNGANO KWA KUFANYA USAFI MACHINGA COMPLEX


WAHAMASISHA MATUMIZI YA MFUMO WA ANWANI ZA MAKAZI

Na Mwandishi Wetu, WMTH - Dodoma.

Watumishi wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Bi. Salome Kessy, leo Aprili 26, 2025 wameadhimisha sherehe za Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kufanya usafi katika Soko la Machinga Complex, jijini Dodoma.

Bi. Salome Kessy amesema, “Sisi kama Wizara tumeona ni vyema kushirikiana na wananchi kwa kufanya usafi katika soko hili, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea maadhimisho ya siku ya Muungano wa Tanzania.”

Zoezi hilo limeambatana na kampeni ya uhamasishaji wa matumizi ya Mfumo wa Anwani za Makazi, ambapo watumishi hao walitoa elimu kwa wananchi mbalimbali waliokuwepo sokoni hapo na maeneo yanayozunguka soko hilo.

Akizungumza mara baada ya zoezi hilo, Bi. Salome Kessy alisisitiza kuwa kila mwananchi anapaswa kufahamu matumizi ya Mfumo wa Anwani za Makazi kutokana na faida zake mbalimbali, ikiwemo utambulisho wa mahali mtu anapoishi pamoja na kurahisisha utoaji na upokeaji wa huduma muhimu.

Aidha, Bi. Kessy aliwahimiza wananchi kuhakikisha wanaufahamu na kuutumia vizuri mfumo huo ili kurahisisha shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wake, Meneja wa Soko la Machinga Complex, CPA. Johnson Kahungu, ameishukuru Wizara kwa kushiriki kufanya usafi na kutoa elimu muhimu kuhusu matumizi ya Mfumo wa Anwani za Makazi kwa wafanyabiashara na wananchi waliopo katika soko hilo.