Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WATUMISHI WA SERIKALI WAASWA KUJILINDA DHIDI YA UHALIFU WA MTANDAONI


Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dodoma.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Uhalifu wa Mtandao kutoka Jeshi la Polisi Tanzania ACP. Joshua Mwangasa amewataka watumishi wa Serikali kuhakikisha wanajilinda dhidi ya uhalifu wa mtandaoni ambao unaweza kuleta madhara makubwa kwa taasisi za Serikali na mtumishi binafsi.

Wito huo umetolewa leo Novemba 7, 2024 wakati wa mafunzo ya matumizi salama ya mtandao kwa watumishi wa Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jakatya Kikwete (JKCC) jijini Dodoma.

Akizungumza katika mafunzo ACP. Mwangasa ametoa rai kwa watumishi wa Wizara hiyo kutumia teknolojia kwa usahihi kwa kuwa wadukuzi wa mtandaoni wameongezeka kwa kasi na njia mbalimbali za ulaghai wa mitandaoni zikiongezeka.

Aidha, amewaasa watumishi wa umma kuwa na utaratibu wa kubadilisha nywila zao za mitandaoni na kusasisha vifaa vyao vya kazi (Simu janja na Kompyuta) mara kwa mara ili kuepuka udukuzi ambao unaweza kuleta athari kwa taarifa za Serikali na taarifa binafsi kwa mtumishi wa Serikali.

Kwa upande wa Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa Mtandao na Teknolojia ya Mawasiliano Mhandisi Emmanuel Urassa amesema kuwa kuwa na matumizi salama ya mtandao ni jukumu la kila mtumishi hasa wakati wa kutekeleza majukumu yao ya kiutumishi pamoja na matumizi ya kawaida ya kijamii na kiuchumi yanayohusisha matumizi ya mtandao.