Habari
WATAALAMU WA POSTA AFRIKA WASHAURIWA KUTUMIA TEKNOLOJIA KUFUNGUA FURSA MPYA

Na Mwandishi Wetu WHMTH, Arusha
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na uchukuzi Zanzibar, Dkt. Mzee Suleiman Mndewa amewataka Wataalamu wa masuala ya Posta Afrika, kutumia vyema maendeleo ya teknolojia katika kuwezesha sekta hiyo kufungua fursa mpya za kiuchumi na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi katika nchi hizo.
Dkt. Mndewa amesema hayo Tarehe 03 Juni, 2024 mkoani Arusha wakati akifungua Vikao vya Kamati za wataalamu wa masuala ya Posta kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) ikiwa ni vikao vya utangulizi kabla ya Mkutano wa 42 wa Baraza la Utawala la PAPU litakalofanyika Juni 11 hadi 12 jijini humo.
Amesema kuwa nchi za Afrika ili ziweze kufanikiwa zaidi katika masuala ya Posta na kuendana na kasi ya ukuaji wa Biashara Mtandao, ni wajibu wao kwa pamoja kama nchi wanachama kuhakikisha kila mmoja anashiriki katika uchumi wa kidigitali.
"Kupitia mkutano huu ni wajibu wetu kuhakikisha tunatafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili nchi wanachama, kwani bado zipo changamoto katika nchi za Afrika ikiwemo miundombinu na teknolojia ambazo zinahitaji kupatiwa ufumbuzi ili kurahisisha mawasiliano kwa haraka," amesema Dk.Mndewa.
Amebainisha kuwa ni vema nchi za Afrika kwa umoja wao zikahakikisha zinatumia teknolojia ili kupunguza gharama na kutimiza malengo ya nchi waliyojiwekea kama nchi.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bi. Salome Kessy amewataka washiriki wa vikao hivyo kuhakikisha majadiliano yao yanazaa matunda na ushauri wao ukawe na matokeo chanya.
“ ...tushirikiane kwa pamoja kutumia uwezo wa sekta ya posta, kuhakikisha kwamba tunajenga mustakabali wa kidijitali, jumuishi na endelevu kwa manufaa ya Waafrika wote,” amesema Bi Salome
Amewaalika washiriki wa mkutano huo kwa ujumla kufurahia mandhari ya jiji la Arusha na viunga vyao na kuitumia vizuri fursa ya uwepo wao nchini kutembelea vivutio vya kitalii ikiwemo Mbuga za Wanyama.
Naye Katibu Mkuu wa PAPU, Dkt. Sifundo Chifu Moyo amesema kuwa, zipo changamoto kadhaa zinazokabili sekta ya Posta zinazowafanya wateja kutokuwa na furaha lakini kwa sasa kwa asilimia kubwa viongozi wa nchi hizo wameanza kuzitafutia ufumbuzi.
Ametaja moja ya changamoto kuwa ni kutikisika kwa Mauzo ya Hisa katika Soko na kushuka kwa mapato hivyo Vikao vya Kamati hizo za Wataalamu vinatarajiwa kutoa majawabu ya namna Teknolojia inavyoweza kuwa suluhu ya changamoto hizo ili kurejesha imani ya wananchi katika sekta hiyo.
“Kama wote mnavyoelewa kwamba teknolojia haimilikiwi na mtu yeyote, kwa hiyo kila mmoja anayo fursa ya kuitumia vizuri teknolojia ili kujikwamua kiuchumi na sekta ya Posta haipaswi kuwa nyuma, kwa sasa Postaa inaichukulia teknolojia kwa uzito mkubwa na ipo kwenye sera zake na ina hakikisha inapeleka teknolojia karibu zaidi na wananchi”, amesema Dkt. Moyo.
Amesema anayo furaha kwani baada ya miaka arobaini tangu ni kwa mara ya kwanza mkutano huo unafanyika katika jengo la PAPU ambalo ni moja ya vitega uchumi na kielelezo cha uwepo wa PAPU, na litadumu kwa miaka mingi ijayo kuonyesha uhai wa sekta ya Posta.
Awali kabla ya ufunguzi huo, Postamasta Mkuu, Bw. Maharage Chande amesema kuwa, mchango wa posta ni kuhakikisha sheria, kanuni na Sera zinasaidia kufanya maboresho mbalimbali katika sekta ya Posta sambamba na kusaidia biashara na uchumi katika nchi za Afrika.
"Tunataka kuzungumza kwa karibu na kuangalia namna tutaweza kufanya biashara kwa urahisi kutoka Kusini kwenda Kaskazini, mtagundua biashara kubwa inatoka Kaskazini yaani nchi za Ulaya kuja Kusini, lakini lazima tuondoke kwenye utaratibu huo, na tunataka kuhakikisha kanuni zinafuatwa katika kufanikisha biashara hiyo," amesema.
Chande amesema kuwa, ili kufanya maboresho katika masuala ya bima, Posta kwa sasa inasisitiza matumizi ya Akili Mnemba (Artificial Intelgence), wanajitahidi sana katika kuhakikisha hawatumii tena barua kama zamani hivyo wanakimbizana kupokea teknolojia ili waweze kutimiza malengo yao .
"Sekta ya posta bado ina mchango mkubwa katika uchumi na maendeleo kwa kuzingatia masuala ya utawala ikiwemo ajenda ya kupokea na kuifanyia kazi matumizi ya akili mnemba yaani (Artificial intelligence), katika Hali hiyo ipo haja kwa mataifa haya kuzidi kuimarisha shughuli za kibiashara ili kukuza uchumi wa mataifa haya pamoja na ulipaji Kodi" amesema Posta masta Mkuu Maharage Chande.
Vikao vya Kamati za Wataalam wa masuala ya Posta, ni utangulizi wa Mkutano wa 42 wa Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika ukiwakutanisha wataalamu mbalimbali kutoka mataifa zaidi ya 15 wanaojadili Mikakati, Kanuni na Sera za kuboresha sekta hiyo kwa manufaa ya mataifa wanachama.
Maafisa bajeti wa kutoka katika Idara na Vitengo vya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wameweka kambi kazi Mkoani Morogoro kwa wiki nzima kuanzia tarehe 27 Mei 2024 kwa ajili ya kuandaa mpango wa manunuzi wa Wizara hiyo na kuupandisha katika mfumo wa manunuzi wa NeST.
Akizungumza wakati wa kikao kazi hicho, Mkurugenzi wa Kitengo cha Manunuzi cha Wizara hiyo, Bi. Kijoli Said ametoa rai kwa maafisa bajeti kuhakikisha mpango unaoandaliwa unatekelezeka ipasavyo kwa kila Idara au Kitengo kufuata taratibu wakati wa kuanzisha mchakato wa manunuzi ya bidhaa au huduma katika ofisi za umma.