Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

Wataalamu wa Korea Exim Bank Wakagua Eneo la Ujenzi wa Chuo Mahiri cha TEHAMA


Ujumbe kutoka Korea Exim Bank ukiongozwa na Naibu Mkuu wa benki hiyo nchini (Deputy Chief), Bw. Wang Kim, ukiambatana na msanifu majengo pamoja na wataalamu wengine kutoka benki hiyo,  umetembelea eneo la ujenzi wa Chuo Mahiri cha TEHAMA (National Digital Technology Institute – NDTI) lililopo Nala, jijini Dodoma, kwa lengo la kujionea maendeleo ya maandalizi ya mradi na kufanya tathmini ya awali ya eneo litakalojengwa chuo hicho.

Katika ziara hiyo, ujumbe huo ulifanya ukaguzi wa eneo la mradi kwa kushirikiana na Mtaalamu wa Usimamizi wa Mradi wa NDTI, Mhandisi Dkt. Seleman Arthur, pamoja na wataalamu wa Tathmini ya Athari kwa Mazingira na Jamii (Environmental and Social Impact Assessment – ESIA) na wataalamu wa usanifu majengo.

 

Timu ya wataalamu ilipata fursa ya kutathmini hali halisi ya eneo la mradi na kujadiliana kuhusu masuala mbalimbali ya kiufundi yatakayowezesha utekelezaji wa mradi kwa kuzingatia viwango vya usanifu, uhifadhi wa mazingira na mahitaji ya chuo hicho, ambacho kinatarajiwa kuwa kitovu cha maendeleo ya teknolojia ya kidijitali nchini.

 

Kwa sasa, mradi unaendelea na hatua za awali za maandalizi zinazojumuisha usanifu wa majengo, tathmini ya athari kwa mazingira na jamii (ESIA), pamoja na maandalizi ya upatikanaji wa fedha kupitia ushirikiano na Korea Exim Bank.

 

Mradi wa Chuo Mahiri cha TEHAMA (NDTI) unatarajiwa kuwa chachu ya kukuza ujuzi, ubunifu na maendeleo ya teknolojia ya kidijitali nchini, huku maandalizi yanayoendelea yakilenga kuhakikisha ujenzi wake unaanza kwa misingi imara ya kitaalamu, kimazingira na viwango vya kimataifa.