Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WATAALAMU 22 WAMEONDOKA KWENDA INDIA KWA AJILI YA MAFUNZO YA MIFUMO YA KIDIJITALI


Na. Juma Wange- WHMTH.

Wataalamu 22 kutoka taasisi mbalimbali za serikali na sekta binafsi ikiwa ni pamoja na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Benki Kuu ya Tanzania(BOT), Wizara ya Fedha, Vodacom, NIDA, RITA, Umoja wa Benki (TBA), Baraza la Taifa la Biashara  TNBC wameondoka Novemba 18, 2023 kwenda nchini India kujifunza teknolojia na masuala muhimu  ya kuboresha mifumo ya kidigitali nchini. Juhudi zinaendana na malengo ya Serikali kufikia uchumi wa kidijitali na kuwarahisishia wananchi kupata huduma za msingi.


Akizungumza Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa uendelezaji wa mifumo na Huduma za TEHAMA   kutoka Wizara ya Habari,Mawasiliano na  Teknolojia ya habari, MOHAMED ABDI MASHAKA amesema lengo la safari hiyo ni kwenda kujifunza namna ya kuoanisha mifumo ya Serikali.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara Tanzania-TNBC DKT. GODWILL WANGA na  Mkurugenzi wa Mifumo ya TEHAMA kutoka mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa-NIDA- Bi Connie FRANCIS wameeleza matokeo yanayotarajiwa kupatikana nchini mara baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo ni pamoja na kujifunza namna mbalimbali ya matumizi ya Jamii Namba kuwezesha  utambuzi kidijitali.

Kulingana na takwimu za sasa, Tanzania ina takriban zaidi ya asilimia 50 ya watu waliochini ya umri wa miaka 18, matumizi ya Jamii Namba yanalenga kuweza kuwatambua wananchi kuanzia umri wa miaka 0. 

Hivyo Nchi ya India imechaguliwa kwenda kujifunza teknolojia za namna gani wamefanikiwa kufanya usajili wa kidijitali ukizangatia wana idadi kubwa ya watu. Hii itasaidia kutupa fursa ya kuboresha mifumo ya utambuzi nchini na kuwawezesha wananchi kutumia taarifa zao za utambulisho mara moja kwani mifumo itaunganishwa na kubadilishana taarifa.

Mafunzo hayo yamedhaminiwa na Serikali ya Tanzania chini ya Mradi wa Tanzania ya Kidijitali na yatafanyika kwa kipindi cha wiki moja kisha wataalamu hao kurejea Nchini.