Habari
WATAALAM WA KOREA KUSINI WAWASILISHA MICHORO YA USANIFU WA JENGO LA CHUO MAHIRI CHA TEHAMA KWA WIZARA YA HABARI

Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla amekutana na wataalamu kutoka Muungano wa Kampuni ya Chuo kikuu cha Hanyang cha Korea Kusini waliofika katika ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwasilisha michoro ya usanifu wa jengo la Chuo Mahiri cha TEHAMA (DTI).
Wataalam hao wakiongozwa na Meneja wa Mradi wa Upembuzi yakinifu wa Chuo Mahiri cha TEHAMA Prof. Taejoon Park kutoka katika chuo kikuu cha Hanyang wamewasilisha michoro ya 3D ya chuo hicho kinachotarajiwa kujengwa katika eneo la Nala, jijini Dodoma leo tarehe 04 Oktoba, 2024.
Prof. Park kwa kushirikiana na Prof. Cha Yong Wook kutoka ndaki ya usanifu na uhandisi katika chuo kikuu cha Hanyang, wamewasilisha na kumpitisha Katibu Mkuu Abdulla kwenye muonekano na aina ya majengo yatakayojengwa katika chuo hicho.
Michoro hiyo inawasilishwa baada ya Chuo hicho kufanya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Chuo Mahiri cha TEHAMA ambacho ujenzi wake utafadhiliwa na Serikali ya Korea kupitia benki ya Exim.