Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WATAALAM WA FEDHA NA UKAGUZI WA NDANI WAJENGEWA UWEZO


Na Mwandishi wetu, Pwani

Wataalam wa Fedha na Ukaguzi wa Ndani wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo wamekutana mkoani Pwani kwa lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu yao pamoja na kujifunza mifumo mbalimbali itakayorahisisha na kuwawezesha kutekeleza majukumu hayo kwa ufanisi.  

Mafunzo hayo yaliyoanza jana, yameendelea hii leo tarehe 28 Februari, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano uliopo katika Shule Kuu ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere, iliyopo Kibaha, mkoani Pwani.ambapo washiriki walipata nafasi ya kujifunza mifumo mbalimbali itakayorahisisha utendaji kazi wao wa kila siku katika taasisi wanazohudumu. 

Washiriki hao wamepata elimu juu ya namna ya kufunga Hesabu kwa kutumia mifumo ya Kimataifa ambayo ni Mfumo wa Kupima masuala ya Uhasibu katika Sekta ya Umma kwa Viwango vya Kimataifa  (IPSAS) na Mfumo wa Utoaji wa Taarifa za Fedha kwa Viwango vya Kimataifa (IFRS) kutoka kwa Mtaalamu wa Hesabu na mwakilishi wa Kamati ya Uteuzi katika Bodi ya  Wahasibu Duniani (IFAC), CPA. Dkt. Neema Kiure.

Mafunzo hayo ya siku tatu, yanaratibiwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 29 Februari, 2024.