Habari
WATAALAM 450 WA TEHAMA KUPATIWA MAFUNZO YA MUDA MFUPI YA TEKNOLOJIA ZINAZOIBUKIA
Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Zanzibar
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali imezindua programu ya mafunzo ya muda mfupi katika fani za TEHAMA kwa wataalam wa TEHAMA 450 kutoka Serikalini kwa lengo la kuongeza ujuzi wa wataalam hao hasa katika teknolojia zinazoibukia.
Mafunzo hayo yamezinduliwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Bw. Juma Mkomi leo Oktoba 28, katika hafla fupi iliyofanyika katika Taasisi ya Teknolojia ya India (IIT Madrasa), Zanzibar
Hafla hiyo ya uzinduzi ilienda sambamba na utiaji saini wa mashirikiano ya utoaji wa mafunzo hayo baina ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Taasisi ya Teknolojia ya India (IIT Madrasa), Zanzibar
Akizungumza katika hafla hiyo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Nicholaus Mkapa amesema kuwa vipaumbele vya Serikali ni kukuza vipaji na taaluma ya TEHAMA katika ngazi zote za elimu ambapo kupitia Wizara hiyo vyuo mahiri viwili vya TEHAMA vitajengwa Dodoma na Kigoma.
Ameongeza kuwa, kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, vituo vya ubunifu nane vitajengwa katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Mbeya, Tanga, Dodoma, Lindi, Dar es Salaam na Zanzibar ambavyo vitakuwa msingi wa kukuza vipaji vya vijana katika sekta yaTEHAMA.
Aidha, Bw. Mkapa amesema kuwa malengo ya Serikali ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha TEHAMA kwa kuwa na wataalamu na wabunifu wabobefu kwa ngazi za Kimataifa kupitia utekelezaji wa Mkakati wa miaka 10 wa Uchumi wa Tanzania ya Kidijitali.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Mkomi amewataka Wakuu wa Idara za TEHAMA nchini kuwa wabunifu na wavumbuzi wa teknolojia zinazoibukia na kuishauri vema Serikali kwa kuainisha mapungufu yaliyopo ili Serikali iangalie uwezekano wa kutafuta nafasi za mafunzo zaidi kwa kushirikiana na taasisi za ndani na nje ya nchi.
Akitoa taarifa ya mafunzo hayo, Mratibu wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, Bw. Bakari Mwamgugu amesema mradi huo unafadhili mafunzo kwa wataalam 500 baada ya tathmini kufanyika na kuona kuna upungufu wa wataalam wa TEHAMA kwenye teknolojia zinazoibukia.
Amesema kupitia mradi huo bajeti ya dola za marekani milioni 5.2 zimetumika kufadhili wataalam 50 kupata mafunzo ya muda mrefu na wataalam 450 kutoka taasisi za Serikali za Tanzania Bara na Zanzibar wamelengwa kupatiwa mafunzo ya muda mfupi yaliyozinduliwa rasmi leo Oktoba 28, 2024.