Habari
Wananchi waomba Elimu zaidi kuhusu Anwani za Makazi

Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dodoma
Wakati Wiki ya Utumishi wa Umma ikihitimishwa, wananchi mbalimbali wameiomba Serikali kutoa elimu zaidi kuhusu Anwani za Makazi na umuhimu wake pamoja na Barua ya Utambulisho hasa katika ngazi za Kata na Vijiji nchini.
Wito huo umetolewa na wananchi mbalimbali waliotembelea Banda la Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, katika maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Wananchi hao kwa nyakati tofauti wamekiri kutouelewa mfumo wa Anwani za Makazi unavyotumika na manufaa yake kwa umma na kuiomba Serikali kuongeza nguvu katika kuelimisha hasa kwa kuwatumia watendaji wa kata.
Akitoa ufafanuzi wa Mfumo wa anwani za makazi kwa baadhi ya wananchi hao Bi. Janeth James amesema Anwani za Makazi ni miundombinu inayotambulisha mahali halisi, mtu ama kitu kılıp o, iwe ni nyumbani, ofisini au eneo la biashara.
“Kutokana na maendeleo ya teknolojia miundombinu hii huambatanishwa na mifumo ya kidigitali ili kuimarisha utendaji kazi na ufanisi katika utekelezaji na matumizi ya Mfumo,” amesisitiza Bi Janeth.
Kuhusu Barua ya Utambulisho wananchi hao wamekiri kwamba baada ya kupata ufafanuzi wameelewa lakini bado haufahamiki kwa wananchi wa kawaida na hivyo ni muhimu elimu kuwafikia ili wengi waweze kuutumia.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yalianza tarehe 16 hadi 23 Juni, 2024 yakiongozwa na kaulimbiu isemayo “Uhusiano kati ya uwezeshaji wa vijana na usimamizi wa masuala ya uhamiaji: Kujenga utamaduni wa Utawala Bora, matumizi ya TEHAMA na ubunifu katika utoaji wa Huduma Jumuishi.”