Habari
Wananchi Wanufaika na Elimu ya Kidijitali Kupitia Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inaendelea kutumia Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma mbalimbali za TEHAMA zinazochangia na kurahisisha maisha yao na kuboresha upatikanaji wa huduma.
Mojawapo ya maeneo yanayovutia wananchi wengi ni Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA), ambapo wananchi wanasajiliwa na kuelimishwa kuhusu matumizi ya mfumo huo pamoja na namna ya kupata Barua ya Utambulisho kwa njia ya kidijitali. Kabla ya kuanzishwa kwa Mfumo wa Anwani za Makazi, wananchi wengi walikuwa wakitumia alama zisizo rasmi kama misikiti, makanisa, miti mikubwa, maduka au majengo maarufu kuelekeza wageni kufika katika maeneo mbalimbali.
Hali hiyo ilisababisha ugumu wa kutambua maeneo kwa usahihi, kuchelewesha utoaji wa huduma na wakati mwingine kusababisha wananchi kushindwa kufikiwa kwa urahisi.
Kupitia utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi, Serikali imeweka msingi imara wa utambuzi wa maeneo kwa kutumia majina ya mitaa na namba za nyumba, hatua ambayo imeongeza usahihi wa maelekezo na kurahisisha wananchi, wawekezaji na watoa huduma kufika katika maeneo mbalimbali bila changamoto.
Sambamba na hilo, mfumo wa NaPA umeimarisha utoaji wa huduma za kidijitali kwa kuwawezesha wananchi kupata kwa urahisi Barua za Utambulisho wa Anwani za Makazi zinazotumika katika kupata huduma mbalimbali za Serikali na sekta binafsi.
Katika eneo la usalama mtandaoni, wananchi wanapatiwa elimu kuhusu namna ya kujikinga dhidi ya uhalifu wa kimtandao unaozidi kuongezeka kutokana na matumizi makubwa ya teknolojia za kidijitali. Wananchi wamekuwa wakipoteza fedha na taarifa muhimu kutokana na utapeli unaofanyika kupitia simu za mkononi, mitandao ya kijamii na viunganishi vya udanganyifu vinavyotumwa kwa njia mbalimbali za mawasiliano.
Kupitia elimu ya Usalama wa mtandao inayotolewa na wataalamu wa Wizara, wananchi wanahimizwa kuhakiki taarifa kabla ya kuzitumia, kutofungua viunganishi visivyoaminika na kulinda taarifa zao binafsi wanapotumia huduma za mtandaoni. Elimu inayotolewa inatarajiwa kuongeza uelewa wa wananchi na kupunguza kwa kiasi kikubwa matukio ya utapeli wa mtandao.
Kupitia maadhimisho hayo, Wizara inaendelea kutekeleza dhamira ya Serikali ya kujenga Tanzania ya Kidijitali kwa kuhakikisha wananchi wanapata elimu, maarifa na huduma zinazowawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali na kunufaika na maendeleo ya TEHAMA nchini.
