Habari
WANANCHI MBEYA WAPOKEA VYEMA ZOEZI LA UHAKIKI WA ANWANI ZA MAKAZI

Na Mwandishi Wetu, WMTH – Mbeya
Halmashauri ya Jiji la Mbeya inaendelea na zoezi la usajili na uhakiki wa taarifa za Anwani za Makazi, ambapo wananchi wa Kata ya Ilomba na Isyesye wamelipokea vizuri zoezi hilo kwa kuutambua mfumo wa Anwani za Makazi kuwa msaada mkubwa katika shughuli zao za kila siku.
Mtendaji wa Kata ya Ilomba, Bw. Nicholaus Kamwela, amesema mafunzo yaliyotolewa awali pamoja na maandalizi mazuri na kutoa taarifa kwa wamiliki wa nyumba mapema yametatua baadhi ya changamoto na kuongeza kasi na ufanisi wa utekelezaji wa zoezi hilo.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Kata ya Isyesye, Bw. Moses Nyondo, amesema wananchi wengi wameupokea vyema mfumo huo licha ya baadhi yao kuwa na hofu ya awali kwamba taarifa zao zingetumika kwa malengo mengine.
Bw. Nyondo alifafanua kuwa baada ya maelezo ya kina na uhamasishaji kwa wananchi yamewajengea uelewa na kuongeza ushirikiano, huku wakitambua manufaa ya mfumo huo katika huduma za kijamii na kiutawala.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Kagera, Bi. Salome Mnyema, ameeleza changamoto zinazojitokeza kuwa ni kuwakosa baadhi ya wananchi katika makazi yao kutokana na shughuli za kazi na wengine kukosa namba za NIDA, lakini amesema jitihada zinaendelea kuhakikisha kila mkazi anafikiwa.
Zoezi la usajili na uhakiki wa Anwani za Makazi linaendelea katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Mbeya. Viongozi wa kata na mitaa wanaendelea kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu ili kuhakikisha utekelezaji wake unakamilika kwa ufanisi na kutoa manufaa yaliyokusudiwa.