Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WANANCHI MBEYA WAFURAHISHWA NA MANUFAA YA MFUMO WA ANWANI ZA MAKAZI


Na Mwandishi Wetu, WMTH – Mbeya

Zoezi la usajili na uhakiki wa taarifa za Anwani za Makazi katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya limepokelewa kwa mwitikio chanya kutoka kwa wananchi wa Kata ya Ruanda, ambao wamebainisha kuwa mfumo huo umekuwa msaada mkubwa katika maisha yao ya kila siku.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Soko, Kata ya Ruanda, Aliko Mwakalinga, alisema mfumo wa Anwani za Makazi umeondoa changamoto kubwa ya utambuzi wa maeneo na makazi.

“Faida kubwa tuliyoipata ni uwepo wa barabara zenye majina na vibao vya namba kwenye kila nyumba. Hii imeondoa ugumu wa kuelekeza wageni kwa maneno pekee. Sasa mtu akipewa jina la mtaa na namba ya nyumba, anafika moja kwa moja bila usumbufu,” alisema Mwakalinga.

Aidha, aliongeza kuwa mfumo huo unawawezesha wananchi kutambulika rasmi, jambo ambalo limekuwa msaada mkubwa hata kwa wanafunzi na wakazi wengine wanapohitaji barua au nyaraka za utambulisho.

Naye mkazi wa Mtaa wa Soko, Feda John, alisema Anwani za Makazi zimekuwa nyenzo muhimu katika urahisi wa kufika makazi ya watu pamoja na kurahisisha huduma mbalimbali kufika moja kwa moja majumbani.

Zoezi la uhakiki wa Anwani za Makazi litafanyika kwa siku 12 katika jiji la Mbeya, chini ya uratibu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), ambapo wananchi wameonesha mwamko na mapokeo Chanya ya zoezi hilo huku wakielezea manufaa ya mfumo huo katika kuboresha shughuli za kijamii na kiuchumi.

Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Soko, Kata ya Ruanda, Bw. Aliko Mwakalinga akizungumza na mwananchi ili kuhakiki taarifa zake za makazi