Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WANAHABARI WASISITIZWA UZALENDO NA MAADILI YA TAALUMA KATIKA UJENZI WA TAIFA


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema wanahabari wana mchango mkubwa katika ujenzi wa Taifa na wanaweza kutoa mchango mkubwa zaidi iwapo watafanya kazi kwa kuzingatia uzalendo, weledi  na maadili ya taaluma.

Rais Mwinyi ameyasema hayo alipokuwa akihutubia wanahabari na wadau wa habari zikiwemo taasisi za kitaifa na kimataifa katika maadhimisho ya miaka 30 ya siku ya Uhuru wa vyombo vya Habari Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika visiwani Zanzibar, tarehe 3 Mei 2023.

Amesisitiza kuwa wanahabari wasipofuata misingi ya taaluma na kujiingiza kwenye propaganda za kichochezi huwa chanzo cha machafuko na kufifisha jitihada za maendeleo hata kuhatarisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa kama ilivyoonekana kwa baadhi ya nchi duniani.

Rais Dkt. Mwinyi ametoa rai kwa wanahabari kutumia siku ya uhuru wa vyombo vya habari kutafakari umuhimu wa kuwa wazalendo kwa nchi na kutambua kuwa hakuna uhuru usio na mipaka na hakuna uhuru bila wajibu.

 “Maadhimisho haya yatumike kama fursa ya kuweka mkazo katika uhuru wa kujieleza ndani ya ajenda ya jumla ya haki za binadamu na haki nyingine”, amesisitiza Rais Dkt. Mwinyi.

Ameongeza kuwa “Kwa upande wa Serikali kupitia Wizara husika za pande zote mbili za Muungano napongeza jitihada za kukuza uhuru lakini pia tusisite kusimamia vyombo vya habari kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo”.

Naye Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kukuza uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza ambapo katika kipindi cha miaka miwili hakuna chombo cha habari kilichofungiwa.

Ameongeza kuwa kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) usajili wa vyombo vya habari umeongezeka kutoka kituo kimoja cha redio na magazeti 10 baada ya uhuru wa Tanganyika hadi kuwa na magazeti 312, redio 218, televisheni 68, redio za kimtandao 8, televisheni za mtandao 391, blog na majukwaa 73 na cable operators 53 waliosajiliwa.

Naibu Waziri Kundo amebainisha dhamira ya Serikali ya kukuza uhuru wa vyombo vya habari ni pamoja na mchakato wa marekebisho ya sheria ya huduma za habari namba 12 ya mwaka 2016. Marekebisho hayo yamewasilishwa na kusomwa Bungeni kwa mara ya kwanza kupitia muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali mwezi Februari mwaka huu.