Habari
WANAFUNZI WA CHUO CHA MIPANGO WAPIGWA MSASA MATUMIZI YA MFUMO WA ANWANI ZA MAKAZI

Na Mwandishi Wetu, WMTH, Dodoma.
Wataalamu wa Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, wakiongozwa na Mkurugenzi wa Huduma za Mawasiliano wa Wizara hiyo, Bw. Mulembwa Munaku, tarehe 2 Februari 2025 walijengea uwezo wanafunzi wa Chuo cha Mipango jijini Dodoma kuhusu matumizi ya mfumo wa Anwani za Makazi.
Akizungumza mara baada ya kufungua mafunzo hayo, Bw. Munaku alisema kwamba Wizara hiyo imeanzisha utaratibu wa kutoa mafunzo kuhusu mfumo wa Anwani za Makazi, na kwa sasa wameanza na vyuo vikuu vilivyopo jijini Dodoma. Tayari mafunzo hayo yamefanyika katika Chuo Kikuu cha Dodoma, na leo yanafanyika katika Chuo cha Mipango.
Bw. Munaku alisema mfumo huo una faida nyingi kwa wanafunzi katika shughuli zao za kila siku, ikiwemo ufahamu wa maeneo pamoja na huduma zinazozunguka, na pia kurahisisha upokeaji wa mizigo na vifurushi.
Aidha, Bw. Munaku alisema kwamba elimu hiyo inatolewa kwa wanafunzi ili kuufahamu vizuri mfumo huo, na hivyo kuweza kuwarahisishia huduma za kila siku pamoja na kuelimisha wengine pindi watakapoanza kazi katika maeneo yao ya mipango miji.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Idara ya Mipango na Mazingira kutoka Chuo cha Mipango Dodoma, Dkt. Francis Mbowe, alishukuru Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kutoa mafunzo hayo kwa wanafunzi hao ambao ni wataalam wa mipango na maendeleo.
“Nimefurahi ujio wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika kutoa mafunzo ya Anwani za Makazi kwa wanafunzi hawa. Wanafunzi hawa wanaandaliwa kuwa wataalam wa mipango na maendeleo, hivyo kupata elimu hii ya Anwani za Makazi kutawasidia kufanya majukumu yao kwa ufanisi,” alisema Dkt. Francis.
Bw. Munaku alitumia mafunzo hayo kuwa kuwakaribisha Wanafunzi hao katika maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi yatakayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma kuanzia tarehe 6 hadi 8 Februari, 2025.