Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WALIMU 300 WA SEKONDARI NCHINI KUPATIWA MAFUNZO YA TEHAMA


Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dar es Salaam

Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia inaendelea  kuhakikisha inaziba pengo la kidijitali kwa kuwapatia walimu wa shule za Sekondari mafunzo ya TEHAMA kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, hususan shule za vijijini ili kuboresha elimu kupitia teknolojia.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb) amesema hayo Oktoba 7, 2024 akifungua  mafunzo ya TEHAMA kwa walimu 300 wa shule za sekondari katika hafla iliyofanyika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) jijini Dar es Salaam.

Mafunzo hayo yanadhaminiwa na Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na yanaendeshwa na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia (MUST) kilichopo Mbeya, na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambapo kila chuo kimepata washiriki 100.

Waziri Silaa alisisitiza kuwa mafunzo haya ni hatua muhimu katika kuhakikisha walimu wanakuwa na uwezo wa kutumia vifaa vya TEHAMA kwa ufanisi zaidi na kupata ujuzi kufanya marekebisho madogo ya vifaa pindi vinapopatwa na hitilafu, pamoja na kuwasaidia kutumia programu mbalimbali za kidijitali ambazo ni muhimu katika ulimwengu wa sasa wa teknolojia.

Katika jitihada nyingine za Serikali kuhakikisha nchi nzima imeunganishwa na teknolojia ya kidijitali Waziri Silaa ameelezea hatua za utekelezaji wa mradi mkubwa wa kufikisha huduma za mawasiliano vijijini, ambapo jumla ya minara 279 kati ya 758 inayojengwa kupitia ruzuku ya UCSAF imeshawashwa na inatoa huduma ambapo ni sawa na asilimia 36 ya utekelezaji wa mradi wote.

Ameongeza kuwa minara hiyo 758 inajengwa katika kata 713 zenye vijiji 1,407 na ukikamilika kwa asilimia 100 jumla ya wananchi milioni 8.5 watanufaika na huduma hiyo muhimu ya mawasiliano. 

Aidha, Waziri Silaa ametoa rai kwa watoa huduma za mawasiliano walioingia mkataba wa ujenzi wa minara hiyo kukamilisha utekelezaji wa mradi huu kwa sababu hatukusudii kuongeza muda wa ujenzi wa minara pindi muda wa mikataba utakapokwisha ifikapo tarehe 13 Mei 2025. 

Katika hatua nyingine amewataka wakandarasi wote waliopewa jukumu la kujenga minara hiyo kuhakikisha wanatekeleza kwa ufanisi mkubwa na kumaliza kazi hiyo kabla ya muda wa mkataba kumalizika.