Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAFANYAKAZI WASHIRIKISHWE KATIKA MAAMUZI – WAZIRI NAPE


WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye, ameliagiza Baraza la wafanyakazi la Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kuhakikisha wafanyakazi wanashirikishwa katika maamuzi na utekelezaji wa majukumu mengine ya mfuko huo ili kutimiza dhumuni ya Serikali la kufikisha mawasiliano sehemu zote nchini.

Akizungumza leo mkoani Morogoro katika hafla ya uzinduzi wa baraza la wafanyakazi la mfuko wa mawasiliano kwa wote (USCAF) Waziri Nape amesema kuwa watanzania kwa ujumla wao ndio wanaowalipa mishahara kutokana na kodi zao hivyo wanatarajia huduma nzuri na bora hivyo Kila mmoja kwa nafasi yake kulingana na kada tofauti zilizopo ahakikishe kwamba huduma za mawasiliano zinamfikia kila Mtanzania.

“Baraza la Wafanyakazi ni chombo kinachowawezesha wafanyakazi kushiriki katika kupanga na kutekeleza mipango ya Taasisi. Mabaraza ya wafanyakazi hutoa fursa kwa wafanyakazi kushiriki katika maamuzi mbalimbali na kuboresha uhusiano baina ya wafanyakazi na viongozi pamoja na mazingira ya utendaji kazi mahali pa kazi ili kutekeleza kwa ufanisi jukumu la kumfikishia huduma mwananchi”, amezungumza Nape

 

Aidha, Waziri Nape ametoa pongezi kwa Menejimenti ya UCSAF na Chama cha Wafanyakazi cha TUGHE kwa kufanikisha uanzishwaji wa Baraza hilo kupitia Mkataba wa Baraza la Wafanyakazi kwa kuwa ni utekelezaji wa Sheria ya Majadiliano ya pamoja katika Utumishi wa Umma, sura ya 105 na Kanuni za Majadiliano ya pamoja katika Utumishi wa umma za Mwaka 2005

Amesisitiza ushirikishaji, weledi na uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya utumishi wa umma kwa kufuata utaratibu sahihi wa kutoa taarifa za Serikali na kuheshimu usiri unaopaswa kuwepo kwa kuhakikisha kila mtumishi anatunza siri za Serikali.

Awali akitoa salam za Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa niaba ya Katibu Mkuu wakati hafla ya uzinduzi wa baraza la wafanyakazi la mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF) Greyson Msigwa amesema Mfuko kwa kushirikiana na watoa huduma umekuwa na msaada mkubwa katika kuboresha huduma za mawasiliano nchini. Haya ni matokeo ya uwajibikaji wa pamoja wa watumishi wote.

“Mfumo wa Anwani za Makazi umekamilika, tuutumie katika kutekeleza majukumu yetu. Kila mfanyakazi awe na anwani ya makazi lakini pia kwa ofisi zetu ziwe na anwani na ziainishe anwani hiyo mbele ya jengo la ofisi, ni muhimu kushirikiana na watalaam wa Mfumo ili kujumuisha taarifa ambazo zitasaidia na kurahisisha utendaji wa majukumu ya Mfuko, mfano taarifa za minara zinaweza kujumuishwa katika Mfumo ili kuwa na taarifa kiganjani zitakazoonesha idadi ya minara, huduma zinazopatikana, eneo ilipo, na kadhalika, pamoja na taarifa mbalimbali za Mfuko mtakazoona zinafaa, Mfumo wa NaPA unakubali maboresho au nyongeza (module) itakayokidhi mahitaji yenu” amesema Msigwa.