Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WAFANYAKAZI WA POSTA WATAKIWA KUZINGATIA MUDA KATIKA KUTOA HUDUMA


Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Ndg. Mohammed Khamis Abdullah amewataka wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania kuzingatia muda katika kutimiza majukumu yao ili kuendelea kutoa huduma zenye tija kwa wananchi
 
Ameyasema hayo leo tarehe 13 Agosti, 2022, wakati alipokuwa akifungua kikao kazi cha wafanyakazi wa Makao Makuu wa Shirika hilo chenye lengo la kutoa mrejesho wa utendaji kazi wa Shirika kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2021/2022, katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Stella Maris, mjini Bagamoyo
 
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu amewataka wafanyakazi wa Posta kutoa huduma zenye ubora kwa wateja kulingana na muda huku akisisitiza ufanisi na kufuata taratibu za kazi ili kuendelea kutoa huduma stahiki kwa wananchi na kuleta matokeo chanya ndani ya Taasisi
 
“Kaja mteja (Customer Care) unapaswa kumpa huduma kulingana na muda, na siyo unamsimamisha tu, muwajali wateja wenu ili wanufaike na huduma zenu”. Amesema Ndg. Mohammed Khamis Abdullah
 
Aidha, Naibu Katibu Mkuu ameendelea kusisitiza uwepo wa upendo, mshikamano na ushirikiano baina ya wafanyakazi wa Shirika lengo ni kuendelea kuijenga Posta mpya ya kisasa na ya kidijitali kwa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla
 
Vilevile, Ndg. Abdullah ametoa wito kwa Viongozi wa Shirika la Posta Tanzania kuwaongoza kwa haki na kuwajali wafanyakazi kwa kuwapa motisha pale inapobidi, lengo ikiwa ni kuwaongezea nguvu na ari ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii.

Sambamba na hilo, Naibu Katibu Mkuu Ndg. Abdullah ametumia nafasi hiyo kulipongeza Shirika kwa jitihada zake mbalimbali za kuendelea kuboresha huduma zake ili kuendana na maendeleo ya Teknolojia Pamoja na mahitaji ya wananchi.

Kwa upande wa Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Ndg. Macrice Mbodo amemshukuru Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Ndg. Mohammed Khamis Abdullah kwa kufika na kufungua kikao kazi cha Wafanyakazi wa Shirika hilo na kuahidi kutumia kikao hicho kuendelea kuboresha utendaji kazi wa Shirika kwa maslahi mapana ya Taifa.

“Kusanyiko hili mbali ya kutafakari utendaji wetu kwa mwaka 2021/2022, lakini pia kwa pamoja tuelewe mwaka 2022/2023 tunakoelekea wapi hii ni kwa kila mmoja wa wafanyakazi wetu wa makao makuu, ndiyo maana wapo hapa leo, lengo ni kutembea pamoja, kufurahi pamoja na kujenga pamoja”. Alimalizia Ndg. Mbodo